Wednesday, October 9, 2013

Maelfu ya walimu wakabiliana na polisi nchini Brazil

Walimu wakiandamana nchini Brazil
Na Victor Melkizedeck Abuso

Maelfu ya walimu wamekabiliana na polisi nchini Brazil katika jiji la Rio de Janeiro na Sao Paulo, wakati wa maandamano ya walimu wakitaka serikali iwaongezee mshahara.
Makabililano hayo yamezuka baada ya walimu wanaokisiwa kuwa zaidi ya 10,000 kuanza kufanya uharibifu katika majengo ya serikali baada ya maandamano hayo kuanza kwa amani katika barabara za miji hiyo.
Usiku kucha walimu na polisi wamekimbizana katika mitaa ya jijini la Rio huku kukiwa na hali ya wasiwasi kipindi hiki suala la usalama likisalia changamoto kubwa  kwa serikali wakati huu nchi hiyo ikijiandaa kuandaa michuano ya soka ya kombe la dunia mwaka ujao na ile ya Olimpiki mwaka 2016.
Walimu nchini Brazil wamekuwa wakidai nyongeza ya mshahara kwa kipindi cha miezi mwili sasa, miezi minane kabla ya kuanza kwa michuano ya kombe la dunia mwaka ujao.
Serikali nchini Brazil inasema imejaribu kushughulikia maswala ya wafanyikazi wa umma nchini humo hasa katika sekta ya elimu na afya ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kwa kipindi kirefu.
Maandamano ya Jumatatu usiku ndio makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa  katika nchi hiyo katika siku za hivi karibuni ambayo yalianza kwa njia ya amani kabla ya kuzuka fujo.
Wanaharakati nchini Brazil wamekosoa sera za rais Dilma Rousseff kuhusu kutumia fedha nyingi kushughulikia maandalizi ya kombe la dunia na Olimpiki nchini humo badala ya kushughulikia changamoto za watumishi wa umma.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment