Wednesday, October 9, 2013

Waangalizi wa Kimataifa wakosoa Uchaguzi wa wabunge nchini Guinea

Viongozi wa Upinzani nchini Guinea
Na Victor Melkizedeck Abuso

Waangalizi wa Kimataifa walioshiriki katika Uchaguzi wa wabunge nchini Guinea wamesema kuwa Uchaguzi huo haukuwa huru na haki kauli inayokuja kipindi hiki upinzani ukitaka Uchaguzi huo kurudiwa.
Wajumbe wa Umoja wa Mataifa waliokuwa nchini humo wanasema kuwa sheria za Uchaguzi zikivunjwa na hivyo kusababisha dosari nyingi kushuhudiwa wakati wa kupiga na kuhesabu kura hizo.
Tume ya Uchaguzi nchini humo CENI kwa sasa inaendelea kutoa matokeo ya awali ambayo yanatumwa katika Mahakama ya Juu ambayo yatathibitishwa baada ya kumi kwa mujibu wa sheria ya Uchaguzi nchini humo.
Hadi sasa, tume ya Uchaguzi haijatangaza matokeo yote ya mwisho baada ya Uchaguzi huo kufanyika mwishoni mwa mwezi uliopita na wachambuzi wa siasa za Guinea wanasema kuwa chama cha rais Alpha Conde kinaelekea kupata ushindi.
Rais Conde mwenyewe amejitokeza na kukansuha madai ya upinzani na waangalizi wa Kimataifa kuwa zoezi hilo halikuwa huru na haki.
Kwa ujumla, viti vya ubunge 114 vinawania katika Uchaguzi huo huku viti vingine 76 vikitarajiwa kugawanywa kwa usawa katika majimbo yote nchini humo.
Uchaguzi wa Guinea umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara kuanzia mwaka 2010 baada ya Uchaguzi wa rais Conde katika uchaguzi ulionekana wa kuimarisha demokrasia nchini humo.
Mwisho wa uchaguzi wa Ubunge nchini Guinea ulifanyika mwaka 2002 wakati utawala wa Kidikteta Jenerali Lansana Conte, aliyefariki duniani mwaka 2008 baada ya miaka 24 kuwa uongozini.
Mapema mwaka huu maandamano makubwa yalishuhudiwa nchini humo hasa jijini Conakry na kusababisha zaidi ya watu 50 kupoteza maisha yao katika makabiliano ya kisiasa.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment