Thursday, October 10, 2013

Wataalam wa silaha za Kemikali waahidi kuharibu silaha za Syria kwa muda

Ahmet Uzumcu Kiongozi wa shirika la Kimataifa linalopambana na utumizi wa silaha za kemikali duniani
Na Victor Melkizedeck Abuso

Kiongozi wa Shirika la Kimataifa linalopambana na utumizi wa silaha za kemikali duniani Ahmet Uzumcu anasema muda unaosalia kuharibu silha hizo zinazomilikiwa na serikali ya Syria ni mfupi.
Hata hivyo, Uzumcu amekanusha madai kuwa shirika hilo halitafanikiwa kuharibu maeneo ya uzalishaji wa silaha hizo nchini Syria kufikia tarehe 1 mwezi wa Novemba.
Licha ya kuisifu Serikali ya rais Bashar Al Assad kwa kutoa ushirikiano unaohitajika, kiongozi huyo amekariri kuwa ushirikiano zaidi ni muhimu sana ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linakamilika kufikia katikati ya mwaka ujao kama ilivyokubaliwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Tayari wataalam hao wameharibu kiwanda kimoja cha kutengeneza silaha hizo za kemikali wakati huu vikisalia viwanda zaidi ya 20 vinavyotarajiwa kuharibiwa kwa wiki kadhaa zijazo kwa mujibu wa wataalam hao.
Aidha, wanasema kuwa serikali ya Syria inamiliki zaidi ya Tani 1,000 silaha zenye sumu ya Sarin ambazo ni hatari mno na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewataka wataalam hao kuwa makini wanapofanya kazi hiyo kwa kile anachokieleza kuwa ni zoezi ambalo halijawahi kushuhudiwa duniani.
Hatua ya kuharibu silaha hizo za kemikali za Syria lilifikiwa kati ya Marekani na Urusi, na kukubaliwa kuwa zoezi hilo likamilike kufikia tarehe 30 mwezi Juni mwaka 2014.
Awali, Marekani ilikuwa imetishia kuishambulia Syria kijeshi baada ya kuituhumu serikali ya Assad kutumia silaha hizo za sumu dhidi ya wapinzani wake mjini Damascus na kusababisha mamia ya watu kuuawa mwezi Agosti.
Machafuko nchini Syria ambayo yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya miaka miwili sasa yamesababisha zaidi ya watu 100,000 kupoteza maisha na Mamilioni kukimbia makwao kwa mujibu wa takwimu za  Umoja wa Mataifa.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment