Tuesday, November 12, 2013

JK: Vijiji 1,600 kupata umeme karibuni

Rais Jakaya Kikwete.PICHA|MAKTABA 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Geita. Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa Serikali yake inaelekeza nguvu nyingi na kasi mpya katika umeme kwa sababu hakuna nchi iliyopata kuendelea kwa kutumia koroboi ama karabai.
Aidha, Rais Kikwete ametaka vyombo vinavyohusika na kusambaza na kuunganisha umeme katika vijiji mbalimbali nchini kuongeza kasi ya kufanya kazi kwa sababu ni lazima vijiji 1,600 vipate umeme katika muda mfupi.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi alipozungumza na wananchi katika eneo la Buseresere/Katoro, mpakani mwa Wilaya za Geita na Chato, Mkoa wa Geita ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Geita. Buseresere na Katoro ni miji iliyoungana lakini Buseresere iko Wilaya ya Chato na Katoro iko Wilaya ya Geita.
Katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Profesa Kulikoyela Kanalwanda Kahigi alimsifu Rais Kikwete kwa kuendesha nchi vizuri na kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza na mamia ya wananchi kabla ya kuzindua mradi mkubwa wa kusambaza umeme katika vijiji vya Wilaya nne za Mkoa wa Geita na moja ya Mkoa wa Shinyanga alisema umeme utasambazwa katika vijiji 14 vikiwamo 10 vya Wilaya ya Geita.
Umeme huo ni sehemu ya miradi mikubwa ya miundombinu ya umeme, barabara, maji na Uwanja wa Ndege wa Mafia unayogharimiwa na Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Milenia Tanzania (MCA-T).
Mradi huo wa kusambaza umeme katika vijiji vya Wilaya za Geita, Chato na Nyang’hwale mkoani Geita na Msalala (Shinyanga) umegharimu Dola za Marekani 21, 477, 181 (sawa
na Sh.36.3 bilioni) na utanufaisha wateja 3,500 katika maeneo hayo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake imeamua kuelekeza nguvu nyingi katika kusambaza umeme vijijini kwa sababu umeme ndiyo maendeleo.
“Hakuna nchi iliyopata kuendelea duniani kwa kutumia koroboi ama karabai. Nchi zote zilizoendelea zimefanya hivyo kwa kutumia umeme na kuwekeza ipasavyo katika sekta hiyo ya umeme.”
Akijibu malalamiko ya wananchi kuwa usambaza wa umeme huo unachelewa pamoja na kwamba wamelipia kuunganishiwa umeme, Rais Kikwete ameziekeleza taasisi zinazohusika na kazi ya kusambaza na kuunganisha umeme.
“Mmesikia wenyewe malalamiko ya wananchi kwamba kasi ya kuunganisha umeme siyokubwa. Napenda tuongeze kasi kwa sababu tunayo kazi kubwa ya kusambaza umeme katika vijiji 1,600 vya nchi yetu katika muda mfupi ujao. Hivyo, tunongeze kasi ili tuweze kuikamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo.”
Rais Kikwete pia aliwaambia wananchi kuwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya umeme kwa urahisi, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imepunguza ada za kuunganisha umeme kutoka Sh450,000 hadi Sh170,000.
Mapema leo, Rais Kikwete amezindua mradi wa maji wa Masumbwe katika Kijiji cha Shinyanga A, wilaya mpya ambazo ziliundwa na Rais Kikwete mwaka jana.
Mradi huo uliogharimu Sh341milioni ni moja ya miradi ya maji katika vijiji 10 kila mkoa inayogharimiwa na Benki ya Dunia (WB).
Rais Kikwete pia amezindua Wodi ya Wazazi katika Kituo cha Afya cha Kijiji cha Iboya, Kata ya Mbogwe. Mradi huo umegharimu Sh57milioni na ujenzi wa wodi hiyo ni maandalizi ya kukifanya kituo hicho cha afya hospitali mpya ya wilaya mpya ya Mbogwe.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment