Writen by
sadataley
4:05 PM
-
0
Comments
Sehemu ya ramani ya Tanzania inayouonyesha mkoa wa Kigoma ambapo watu
walirusha bomu kwenye daladala na kusababisha vifo. Picha na Maktaba
Na Waandishi Wetu, MwananchiKigoma/Songea/Arusha. Watu watatu wamefariki dunia na wengine
sita kujeruhiwa baada ya mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi, kurusha bomu
ndani ya basi dogo aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitoka Kilelema
kwenda Kasulu, Kigoma.
Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Kijiji
cha Kilelema, Benedicto Mahuta alisema tukio hilo lilitokea saa 11:00
alfajiri kwenye Pori la Kasesema, lililopo kati ya kijiji hicho na Kambi
ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Migongo, Wilaya ya Buhigwe.
Mahuta alisema wakati gari hilo likipita eneo
hilo, mtu mmoja alionekana amesimama katikati ya barabara huku ameshika
bunduki, hali iliyomlazimu dereva kuongeza kasi.
Alisema hatua 15 baada ya kumpita, walimuona mtu
mwingine akiwa amesimama pembeni mwa barabara na baada ya kumpita,
abiria waliokuwa wameketi nyuma ya basi hilo walishtukia kitu kizito
kikitupwa ndani.
Mmoja wa abiria aliamua kukirusha nje lakini kililipuka na kusababisha vifo vya watu wawili na mtoto mdogo.
Mmoja wa abiria walionusurika, Mwalimu wa Shule ya
Msingi Kilelema, Augustino Mkubhaka alisema baada ya mlipuko huo, gari
lilipelekwa katika kambi ya JWTZ kwa ukaguzi.
Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Buhigwe, Samwel
Utonga alisema inasadikiwa kuwa watu waliorusha bomu hilo ni majambazi
wanaotokea nchi jirani.
Dereva wa jaji EACJ auawa
Dereva wa mmoja wa majaji wa Mahakama ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EACJ), Ibrahim Msagati amefariki dunia kwa kupigwa
risasi iliyofyatuka kutoka kwenye bastola ya mlinzi wa jumuiya hiyo.
Tukio hilo lililoibua majonzi na simanzi miongoni
mwa wafanyakazi wa EAC lilitokea jana saa saba mchana muda mfupi baada
ya kikosi cha ulinzi cha Jumuiya kumtia mbaroni mtu mmoja aliyefika
Makao Makuu ya EAC kwa tuhuma ambazo hazikujulikana mara moja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas
alisema tukio hilo ni la bahati mbaya kwani risasi ilifyatuka kutoka
kwenye silaha ya mmoja wa maofisa usalama wa EAC.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma wa EAC,
Richard Otieno-Owora alimtaja ofisa usalama ambaye risasi ilifyatuka
kutoka kwenye bastola yake kuwa ni Jackson Oula.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa
wafanyakazi wa Sekretarieti ya EAC alisema risasi hiyo ilifyatuka wakati
ofisa huyo akijaribu kutoa simu maalumu ya kiusalama waliyotumia kunasa
mawasiliano ya mtu waliyemtia mbaroni ili kuwapa ushahidi polisi
waliokuwa wakichukua maelezo yao.
“Wakati akitoa simu mfukoni, risasi aliyoiweka
chemba wakati wa kumtia mbaroni mtuhumiwa ilifyatuka na kutoboa kiti
alichokalia mfanyakazi mwenzetu na kumpiga mgongoni na kusababisha kifo
chake,” alisema.
Dereva huyo aliajiriwa hivi karibuni na alikuwa akiendesha gari inayotumiwa na Jaji Mfawidhi wa EACJ, Jean-Bosco Butasi.
Amchoma kisu mpenziwe
Mkazi wa Mandepwende, Ally Hassan (29) amelazwa
katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma baada ya kumchoma kisu shingoni
mpenzi wake aliyetambulika kwa jina la Zamda Rashid (19) na kisha
kujichoma kisu tumboni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
alisema tukio hilo lilitokea jana saa tano usiku katika Kijiji cha
Mandepwende baada ya kutokea ugomvi baina yao wakiwa nyumbani kwa
mwanamume huyo.
Alidai kuwa katika ugomvi huo, Ally alimchoma kisu
cha shingo na alipoona ameanguka chini akiwa ametapakaa damu alidhani
ameua, hivyo naye aliamua kujichoma kisu cha tumbo ili kujiua lakini
alipoteza tu fahamu baada ya kupoteza damu nyingi.
“Baada ya kujichoma kisu, wasamaria waliwahi na
kumwahisha katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma ambako yeye pamoja na
mpenzi wake wamelazwa na wanaendelea na matibabu.”
Mihayo alisema polisi wanaendelea kuchunguza tukio hilo na upelelezi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Imeandikwa na Diana Rubanguka (Kigoma); Peter Saramba na Mussa Juma (Arusha) na Joyce Joliga (Songea).
No comments
Post a Comment