Saturday, August 16, 2014

Felishi: Majalada mengi hayana ushahidi


Rais Jakaya Kikwete akimwapisha Mkurugenzi wa Mashtaka, Eliezer Feleshi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis.      
Na Ibrahim Yamola, MwananchiDar es Salaam. Siku moja baada ya kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Eliezer Feleshi amesema majalada mengi ya kesi yaliyo katika ofisi hiyo hayana ushahidi.
Feleshi aliyasema hayo jana kwenye Viwanja vya Ikulu muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaapisha majaji 20 aliowateua Agosti 13 kuwa majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kuhusu madai ya kuwapo majalada mengi ya kesi katika ofisi aliyoiacha yakisubiri kwenda mahakamani, Feleshi alisema:
“Hizo ni hisia tu, hakuna ushahidi kwani yaliyopo hayana ushahidi. Natoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya umma ili viweze kumaliza mapambano dhidi ya rushwa na matukio mengine.”
Aliongeza: “Kwa kipindi cha miaka saba na nusu niliyoapa kuwa DPP niliyoyafanya huko nitayaendeleza tena baada ya kuapa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, hivyo ni mwendelezo wa majukumu ya fani ile ile.”
Katika hali ya utani, Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akisalimiana na Feleshi alimuuliza:“Sijui nikupe pole au pongezi?”
Feleshi alijibu: “Nipe tu pongezi kwani nipo tayari kwa kazi yoyote.”
Naye Jaji Mkuu, Othman Chande alisema Septemba mosi majaji hao wapya watakwenda kupatiwa mafunzo ya wiki tatu katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mkoani Tanga.
Alisema uteuzi alioufanya Rais Kikwete utapunguza upungufu wa majaji hasa katika Mahakama za Mwanza, Dar es Salaam na Tabora.
“Tangu Rais Kikwete aingie madarakani ameweza kuteua majaji 81,” alisema Othman.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment