Writen by
sadataley
6:35 PM
-
0
Comments
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
Na Neville Meena, MwananchiDodoma. Kero za Muungano na taasisi zake
zilizotajwa na mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba zimekuwa zikiwatesa wajumbe wa Bunge Maalumu katika
mijadala ya rasimu ya Katiba inayoendelea kwenye kamati za chombo hicho.
Miongoni mwa maeneo ambayo yametajwa kusababisha
mvutano mkali katika kamati nyingi ni muundo wa Bunge ambao ulitajwa na
Jaji Warioba wakati akiwasilisha taarifa ya Tume kuwa una kasoro nyingi
ambazo zimesababisha malalamiko kutoka kila upande wa Muungano.
Habari kutoka katika vikao kadhaa vya kamati
zinasema baadhi ya wajumbe kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao
walikuwa wakiamini katika muundo wa serikali tatu pamoja na baadhi wa
Kundi la 201, wamesimama kidete wakitaka yafanyike mabadiliko makubwa ya
muundo wa Bunge la Muungano.
“Muundo wanaopendekeza ni kuwa na Bunge la ‘tatu
ndani ya moja’ kwa maana kwamba Spika anakuwa mmoja, lakini huku ndani
kunatolewa fursa za wabunge wa Tanzania Bara kunapokuwa na masuala yao
na wale wa Zanzibar wakutane kwa masuala yao na yale ya muungano basi
wote tukutane,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati Namba Tano.
Ikiwa pendekezo la muundo wa aina hiyo ya Bunge
utakubaliwa, majimbo ya Zanzibar yatakuwa na mwakilishi mmoja mmoja,
tofauti na sasa ambapo kila jimbo lina mbunge anayeshiriki katika Bunge
la Muungano na mwakilishi anayeingia katika Baraza la Wawakilishi.
Watetezi wa muundo huo wanasema pia utajibu kero
mbili zilizotajwa na Jaji Warioba ambazo ni wabunge kutoka Zanzibar
kushiriki katika mijadala ya mambo yasiyo ya muungano na ile ya sheria
zinazopitishwa na Bunge la Muungano kulazimika kupata kibali cha Baraza
la Wawakilishi kabla ya kuanza kutumika visiwani humo.
Kwa upande wa wabunge wa CCM wenye msimamo huo,
wameujenga katika ahadi waliyopewa na viongozi wao kwamba waunge mkono
wazo la kubaki na muundo wa serikali mbili ‘zilizoboreshwa’ hivyo
wanataka mabadiliko kadhaa tofauti na wahafidhina ambao wamekuwa
wakisimamia muundo wa sasa ubaki kama ulivyo.
“Hawa wakubwa wetu sijui vipi, yaani wanataka kila
kitu kibaki kama kilivyokuwa na ikiwa hivyo itakuwa tabu kweli. Ukawa
watapata sifa kwamba walichokisema kuwa lengo letu (CCM) ni kubaki na
mfumo wa sasa kwa kila kitu itakuwa kweli,” alisema mjumbe mwingine wa
Kamati Namba 11.
“Haitakuwa na maana sisi kukaa hapa kwa siku zote
halafu tunakuja na yaleyale, lazima hizo serikali mbili zilizoboreshwa
zionekane kwa watu, ili watuamini kwamba tulibaki hapa kufanya kazi. La
sivyo uamuzi wa kurejea na yaleyale utatuweka pagumu sana hata kwenye
uchaguzi ujao wa 2015.”
Kamati ya uongozi
Suala hilo pamoja na mengine kadhaa yaliyowekwa
kiporo katika baadhi ya kamati kutokana ugumu wake, yalisababisha Kamati
ya Uongozi ya Bunge Maalumu kukutana kwa siku mbili mfululizo (juzi na
jana) kujaribu kuyatafutia ufumbuzi.
Juzi kikao hicho kilikutana kwa saa sita, kuanzia
saa 5:00 asubuhi na kuahirishwa saa 11:00 jioni, lakini kutokana na
kushindwa kumaliza ajenda zake, kilifanyika tena jana kuanzia saa 5:00
asubuhi. Lakini haikuweza kufahamika kuhusu uamuzi wake wa masuala tata
yaliyokuwa yakijadiliwa.
Kaimu katibu wa Bunge la Katiba, John Joel juzi alikiri kuwapo
kwa kikao hicho lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani ajenda zake.
Matokeo ya kikao hicho yanaweza kupelekwa kama ‘maelekezo’ ndani ya
kamati, lakini huenda yakapata upinzani mkubwa kutoka kwa wajumbe ambao
kikanuni wana uwezo wa kuamua kadiri watakavyokubaliana.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema Ijumaa
iliyopita, mjadala katika Kamati Namba 5 uliahirishwa baada ya mjumbe
wake, Paul Makonda kusimama kidete akitaka muundo wa Bunge ufanyiwe
marekebisho tofauti na ulivyo sasa, hoja ambayo iliungwa mkono na
wajumbe wengine kadhaa.
Habari zinasema suala hilo lilisababisha mvutano
mkali kutokana na wajumbe wa Zanzibar kuipinga hasa pale inapoonekana
kwamba nafasi zao za uwakilishi zitapungua kutoka mbili za sasa kwenye
majimbo hadi moja.
“Baadhi yao wanajenga hoja kwamba eti suala hilo
litahatarisha Muungano na sisi tumewaambia yanapokuja mambo ya kwao
wanakubali, lakini likija la upande wa Bara wanaleta sababu. Sisi
hatutakubali katika hili,” alisema mjumbe mwingine wa kamati hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati Namba 5, Hamad Rashid Mohamed
alisema mjadala kuhusu suala hilo ni wa kawaida na kwamba leo
watalifanyia uamuzi wa mwisho kwa maana ya kupiga kura ya mapendekezo.
Hoja nyingine ambayo iliibuliwa na Tume ya Warioba
na ambayo imekuwa ikisumbua vichwa vya wajumbe katika kamati ni nafasi
ya Makamu wa Rais ambayo imekuwa na mapendekezo ya kuwapo kwa nafasi
tatu lakini baadhi yao wakipinga wazo hilo. Jaji Warioba alisema
wananchi wa Zanzibar walilalamika kwamba Rais wao hana nafasi ya
kutambuliwa katika Muungano hivyo walitaka arejeshwe katika nafasi ya
makamu wa Rais.
Hata hivyo, hofu ambayo imeonekana miongoni mwa
wajumbe hasa wanachama wa CCM ni iwapo rais atatoka nje ya chama chao,
hivyo kupendekeza kwamba wawepo makamu watatu, hoja ambayo pia
inapingwa. Hoja hizo zinatarajiwa kushika mjadala wakati kamati nyingine
zitakapoendelea na vikao.
No comments
Post a Comment