Writen by
sadataley
6:45 PM
-
0
Comments
Rais Jakaya Kikwete.PICHA|MAKTABA
Na Ally Mkoreha, MwananchiKilombero. Rais Jakaya Kikwete amezindua miradi
miwili mikubwa ya kiuchumi na kijamii katika Wilaya za Ulanga na
Kilombero, ukiwamo ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa daraja hilo
uliofanyika saa 1.20 usiku, Rais Kikwete alisema daraja hilo
linalojengwa kwa Sh53.2 bilioni, litasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi
katika wilaya jirani zilizokuwa na tatizo kubwa la usafiri kwa muda
mrefu.
Ujenzi wa daraja hilo uliokuwa ukisubiriwa kwa
shauku na wananchi wa wilaya hizo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipata
mateso katika kuvuka mto huo ambao umetanguliwa na madaraja madogo
zaidi ya 16 upande wa Kilombero.
Madaraja hayo ni kwa ajili ya kuunganisha tuta
kubwa litakalounganishwa na daraja hilo refu, likiwa ni moja ya ahadi za
Rais Kikwete alizotoa wakati akiwania nafasi hiyo katika kipindi cha
pili.
Umati wa wananchi wa Kilombero kutoka maeneo ya
karibu mahali linapojengwa daraja hilo, ulihudhuria uzinduzi wa ujenzi
wa daraja hilo na wengi wao wakielezea kufarijika.
Kwa muda mrefu wananchi wa wilaya hizo wamekuwa
wakitumia vivuko na mitumbwi isiyokuwa na uhakika kuvuka katika mto huo,
jambo lililohatarisha usalama wao.
Baadhi ya wananchi, wamewahi kupoteza maisha walipokuwa wakivuka kutoka upande mmoja wa Mto Kilombero kwenda mwingine.
Tatizo hilo pia limekuwa likiathiri jitihada za
wakulima wa mpunga katika wilaya hizo hasa kuyafikia masoko ya zao hilo
kwa sababu ya ugumu wa kuvusha shehena katika mto huo.
“Ujenzi wa daraja hilo sasa ni ukombozi mkubwa
kwetu maana mateso yetu katika kuvuka mto huu, yatakwisha. Tumeteseka na
hakika sasa Serikali imesikiliza kilio chetu,” alisema mkazi wa
Michenga wilayani Kilombero, Adriano Liyonga.
Alisema harakati za kuvuka katika Mto Kilombero,
zimesababisha watu wengi katika wilaya za Ulanga na Kilombero kupoteza
maisha na kwamba kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo kutapunguza kero kubwa
kwa wananchi.
Mkazi mwingine, Juliana Moses alisema:
“Tunamshukuru Mungu, tunaishukuru Serikali yetu kwa kusikiliza kilio
chetu cha muda mrefu kuhusu daraja katika mto huu. Ngoja tufurahi,”
Kauli hiyo iliungwa mkono na nduye Adriano, Aidan
Liyonga aliyesema ujenzi wa daraja katika mto huo utaharakisha zaidi
maendeleo ya kiuchumi katika wilaya hizo.
Mradi mwingine ambao Rais Kikwete aliuzindua jana ni wa umeme vijijini katika Tarafa ya Mwaya, wilayani Ulanga.
Mradi mwingine ambao Rais Kikwete aliuzindua jana ni wa umeme vijijini katika Tarafa ya Mwaya, wilayani Ulanga.
No comments
Post a Comment