Writen by
sadataley
3:18 PM
-
0
Comments
Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe tafsiri hiyo, chini ya
vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba
83 ya mwaka 2011.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es
Salaam imeanza mchakato wa kusikiliza kesi dhidi ya Bunge la Katiba
baada ya kupanga jopo la majaji wa kuisikiliza.
Kesi hiyo namba 28 ya 2014, ilifunguliwa
mahakamani hapo na mwandishi wa habari, Saed Kubenea kupitia kwa Wakili
Peter Kibatala, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiiomba mahakama
hiyo itoe tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hilo.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka
mahakamani hapo jana na kuthibitishwa na Wakili Kibatala, kesi hiyo
imepangwa kusikiliza na jopo la majaji watatu.
Majaji hao ni Agustine Mwarija ambaye ndiye kiongozi wa jopo akishirikiana na Dk Fauz Twaib na Aloysius Mujulizi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vyetu, licha ya
kesi hiyo kupangiwa jopo la majaji hao, hadi jana ilikuwa haijapangwa
tarehe ya kutajwa.
Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe
tafsiri hiyo, chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya
Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka
ya bunge hilo, pia Kubenea amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba
mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri
uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.
Maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda
yaliyopewa namba 29 ya 2014 na maombi ya msingi ya tafsiri ya mamlaka ya
Bunge, yote yalifunguliwa mahakamani hapo chini ya hati ya dharura.
Katika maombi ya msingi, Kubenea anaiomba Mahakama
hiyo itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria hiyo
na pia itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya
Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa
kiwango gani.
Kwa mujibu wa hati hiyo, uamuzi wa kufungua kesi
hiyo kuomba tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge umetokana na mjadala na
mvutano wa kisheria ndani na nje ya Bunge hilo kuhusu mamlaka ya chombo
hicho.
Mjadala na mvutano huo ni iwapo Bunge hilo katika
utekelezaji wa majukumu yake linayo au halina mipaka kwa mujibu wa
vifungu hivyo vya 25 (1) na 25 (2), kiasi kwamba linaweza kuacha
mapendekezo ya Rasimu ya Katiba na kuweka mapendekezo mapya.
Katika kusisitiza mjadala kuhusu mamlaka ya Bunge
hilo, hati hiyo inatoa mfano wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),
katika mkutano wake wa mwaka, ambao kilisema kuwa vifungu hivyo havilipi
Bunge hilo mamlaka ya kubadili rasimu hiyo.Inaeleza kuwa wakati TLS wakitoa msimamo huo, kuna wataalamu wengine wa
sheria wanadai kuwa Bunge hilo linaweza kubadilisha na kuongeza ibara
kadri litakavyoona inafaa bila kujali rasimu hiyo.
No comments
Post a Comment