Writen by
sadataley
6:27 PM
-
0
Comments
Mwenyekiti wa CUF Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa gazeti hili. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Elias Msuya, MwananchiDar es Salaam. Wakati mchakato wa Katiba mpya
unaendelea mjini Dodoma na suala la theluthi mbili likisumbua vichwa vya
wengi, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuwa kura za
wajumbe 14 kutoka Zanzibar ndizo zitauokoa au kuukwamisha mchakato huo.
Profesa Lipumba alikuwa kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi
nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kuhusu mustakabali wa
mchakato wa Katiba baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kususia kuhudhuria vikao.
Kundi hilo lilisusia vikao Aprili 16 kwa madai
kuwa Bunge lilipoteza mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba,
hasa katika suala la muundo wa serikali ya Muungano na kwamba chama
tawala, CCM kiliingiza suala la serikali mbili ambalo halimo kwenye
rasimu hiyo badala ya serikali tatu.
Kutokana na uamuzi wa Ukawa, ambayo inaundwa na
wajumbe kutoka CUF, Chadema, NCCR Mageuzi na baadhi wa kundi la 201
kutoka taasisi mbalimbali za kijamii, kuna shaka kwamba mchakato huo
huenda usifanikiwe kutokana na ukweli kuwa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba inataka uamuzi upitishwe na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara
na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.
Kutokana na utashi huo wa kisheria, Profesa
Lipumba alisema wana uhakika kuwa Katiba haitapita kwa kuwa wanao
wajumbe 14 kutoka kundi la 201 ambao ndiyo tegemeo lao.
“Sisi tunao wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar
wa vyama vyetu ambao hawakwenda hata kwenye vikao. Tukiwajumlisha,
tunahitaji watu 14 kutokana na wale wajumbe 77 (wa Zanzibar) wa Kundi la
201 na kule tuna uhakika wa watu kama 21,” alisema.
“Wapo baadhi waliokwenda kuhudhuria vikao, lakini
tunajua misimamo yao. Tunajua kuna mbinu zinafanyika kuwarubuni, lakini
tunawafuatilia kwa karibu.”
Alisema kuwa Ukawa wana uhakika pia wa kuungwa
mkono na wabunge na wawakilishi wa CCM kutoka Zanzibar katika kutetea
mamlaka ya Zanzibar.
“Kama mnafuatilia mazungumzo ya Baraza la
Wawakilishi, katika malalamiko ya suala la Muungano, mazungumzo ya CUF
na CCM yalikuwa yanafanana na hata ule waraka uliopelekwa bungeni kutoka
CCM Zanzibar ambao sasa wanaukana, unataka mamlaka tatu. Maana yake
nini? Mamlaka ni Serikali,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Hata kura zitakapopigwa, CCM hawawezi kupata theluthi mbili za upande wa Zanzibar. Suala la Katiba ni suala la maridhiano.”
Aitetea Tume ya Jaji Warioba
Huku akitetea uamuzi wa Ukawa kutoka nje ya Bunge
la Katiba, Profesa Lipumba ametaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja
na rasimu iheshimiwe kwa kuwa imefanya kazi kubwa.
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/Katiba/Lipumba--Moyo-wetu-Ukawa-ni-wajumbe-14/-/1625946/2422428/-/jhf03f/-/index.html
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/Katiba/Lipumba--Moyo-wetu-Ukawa-ni-wajumbe-14/-/1625946/2422428/-/jhf03f/-/index.html
No comments
Post a Comment