Writen by
sadataley
7:43 PM
-
0
Comments
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupitia Taasisi za Elimu ya Juu
(wanafunzi), Teddy Ladislaus, akizungumza na waandishi wa habari mjini
Dodoma jana. Kulia ni mwanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma, Mfinanga
Elisante. Picha na Emmanuel Herman
Na Waandishi Wetu, MwananchiDodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
anayedhaniwa kuwa na umri mdogo zaidi, Teddy Ladislaus (22), amesema
kitendo cha Bunge hilo kuendelea na vikao vyake ni kutumia vibaya fedha
za walipakodi na ni ‘dhambi’ ambayo wajumbe wanawatendea Watanzania.
Kwa sababu hiyo, mjumbe huyo kutoka Kundi la
Wajumbe 201, ametaka liahirishwe ili kuokoa fedha hizo kwa kuwa kuna
dalili kwamba Katiba bora haitapatikana kama Rais Jakaya Kikwete
alivyoahidi alipoanzisha mchakato huo Desemba 31, 2011.
Binti huyo anayesubiri kutunikiwa Shahada ya
Kwanza ya Teknolojia ya Habari na Biashara katika Chuo Kikuu cha Mzumbe
baadaye mwaka huu aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba: “Tutakuwa
tumetenda dhambi kubwa ikiwa tutawahadaa mamilioni ya Watanzania kwamba
tutawaletea Katiba bora wanayoihitaji kama alivyosema Mheshimiwa Rais
Kikwete wakati si kweli.
“Ni dhambi ya dhuluma ambayo tunapaswa, siyo tu
kutubu, bali kutubu na kuacha. Nawaomba viongozi wakuu watambue kuwa
Katiba bora itapatikana kwa maridhiano na siyo kwa ushindani na ubabe wa
kisiasa”. Alisema lazima aisemee dhambi hiyo ambayo inaonekana
kupumbaza fikra za walio wengi na kuweka masilahi ya watu wachache
mbele, huku fedha za wananchi zikiendelea kutumika kwa kazi ambayo haina
tija kwa sasa.
“Siwezi kuukana uzalendo wangu na kuogopa gharama
za kusimamia ukweli. Dhamira yangu imeongoza fikra zangu kuamua
kulisemea hili kwa niaba ya wale ninaowawakilisha,” alisema.
Alisema fedha nyingi zinazotumika sasa
zingeelekezwa kutatua changamoto nyingine za kijamii, ikiwamo kuwapatia
mikopo kundi kubwa la wanachuo walio na vigezo, kulipa malimbikizo ya
madai ya watumishi hasa walimu na kugharimia miradi mingine ya
maendeleo.
“Tumefumba masikio na hatutaki kusikia wasia na
kilio cha wananchi na tumefumba macho hatutaki kuona uhalisia wa maisha
ya Watanzania wenzetu, hii siyo sawa hata kidogo,” alisema.
Kauli yake iliungwa mkono na Rais Mtaafu wa Chuo
cha Mipango, Mfinanga Elisante na Rais Mstaafu wa Chuo cha Usimamizi wa
Fedha (IFM), Hemed Ngw’ali ambao aliambatana nao.
“Hakuna haja ya matumizi ya fedha nyingi kiasi
hicho kwa jambo lisilo na tija kwa nchi wakati ni wiki saba sasa
wanafunzi wako katika mazoezi ya vitendo na hawajui hatima yao na
wanawaona watu wakiwa huku Dodoma wakitumia fedha,” alisema Ngw’ali.
Elisante alisema maridhiano kati ya pande mbili zinazokinzana ni muhimu sana katika kufanikisha mchakato wa Katiba.
Ladislaus alisema mgogoro uliopo baina ya makundi
yenye masilahi ya kisiasa ni dhahiri umekwaza mchakato huo, hivyo busara
zitumike kuuahirisha kwa sasa hadi hapo kutakapokuwa na maridhiano na
mwafaka wa kitaifa kuhusu suala hilo.
“Mazunguzo siku zote ni ‘give and take’ yaani
kulegeza msimamo katika baadhi ya hoja badala ya kila upande kushupaa
kwa kile unachokiamini. Tukiwa na nia ya dhati ya kuzungumza,
tukashauriana, tukaridhiana na kukubaliana jinsi ya kutekeleza yale
tuliyoafikiana, basi Taifa litapata Katiba bora hivyo kuondoka katika
mkwamo wa sasa.
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/Katiba/Mjumbe-wa-Bunge-Maalum--Hii-ni-dhambi-kubwa/-/1625946/2419530/-/ssg27ez/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/Katiba/Mjumbe-wa-Bunge-Maalum--Hii-ni-dhambi-kubwa/-/1625946/2419530/-/ssg27ez/-/index.html
No comments
Post a Comment