Wednesday, August 27, 2014

Mkapa: Mgongano wa masilahi utazamwe


Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa akimsikiliza Jaji Mstaafu, Joseph Warioba baada ya kufungua warsha inayojadili mapendekezo ya kutungwa kwa sheria mpya ya kudhibiti mgongano wa maslahi miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma jijini Dar es Salaam jana.Kulia ni Kamshna wa Sekretalieti ya maadili viongozi wa umma, Jaji Susan Kaganda. Picha na Venance Nestory 
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amesema tatizo la mgongano wa masilahi kwa viongozi na watumishi wa umma linahitaji kutazamwa kwa umakini ili kuleta usawa katika utoaji wa uamuzi wa jambo lolote, hasa linalowagusa wananchi.
Wakati Rais Mkapa akisema hayo, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu, Joseph Warioba amesema Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatakiwa kuwa tume kamili itayowachukulia hatua viongozi wasio waadilifu.
Walisema hayo jijini hapa jana katika warsha ya kupokea maoni kuhusu sheria ya mgongano wa masilahi miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma kutoka kwa wadau mbalimbali iliyoratibiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Rais Mkapa alisema Afrika Kusini wamepiga hatua kwa kuanzisha kampuni za udhamini kwa ajili ya kuweka biashara za viongozi wanaokuwa madarakani ikiwa ni namna kuepuka mgongano wa masilahi.
“Tatizo hili linajidhihirisha kwa namna ambavyo wenye mamlaka au watoa uamuzi wanapokuwa na masilahi kwenye jambo fulani wanatumia madaraka yao kujiendeleza binafsi badala ya kutoa kipaumbele kwa umma. Huo ndiyo mgongano wa kimasilahi ambao wengine huingia kwa makusudi au kwa kutokujua, hilo linahitaji kutazamwa kwa umakini mkubwa,” alisema.
Jaji Warioba alisema wakati wakikusanya maoni ya Katiba kutoka kwa wananchi, eneo lililotolewa maoni kwa wingi ni lile la kuboresha maadili ya viongozi wa umma.
“Tumependekeza sekretarieti iwe tume kamili yenye madaraka makubwa ya kutoa uamuzi bila kuingiliwa jambo litakalorejesha maadili kwa viongozi wetu ambayo kama hayapo basi sheria haiwezi kufanya kazi ipasavyo,” alisema.
Jaji Warioba ambaye alifika akiwa amechelewa, alipotakiwa kujitambulisha alisema: “Mimi naitwa Joseph Warioba raia mwandamizi,” maneno yaliyoibua furaha ukumbini huku mshereheshaji wa mkutano huo, Suleiman Madege akisema: “Ndiyo maana nimeshindwa kumtambulisha kwa kuwa ningesema mbili au tatu.”
Awali, Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji Mstaafu Salome Kaganda alisema utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma unahitaji kutazamwa kwa jicho la pekee.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Ibrahim Kaduma alisema: “Serikali inatakiwa kuhakikisha haivifungii vyombo vya habari kwa kuwa ndiyo mhimili wake wa nne, ikifanya hivyo ni uvunjifu wa maadili.” Kamishna wa kwanza wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu William Maina alisema viongozi hawatakiwi kutumia vibaya madaraka.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment