Writen by
sadataley
3:13 PM
-
0
Comments
Rais Jakaya Kikwete
Na Waandishi Wetu, MwananchiZanzibar/Dar/Dodoma/Arusha. Uamuzi wa Rais
Jakaya Kikwete kutaka kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye
wabunge kupitia muungano wao wa Kituo cha Demokrasia (TCD), umeibua
mjadala katika sehemu mbalimbali nchini huku wasomi na wanasiasa wakitoa
angalizo.
Miongoni mwa watu walihojiwa, pamoja na
kukubaliana na uamuzi huo wa kutafuta mwafaka, suala la Bunge kuendelea
na vikao kabla ya maridhiano hayo limeendelea kuiweka Katiba Mpya
njiapanda.
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS), Charles Kibodya amesema, “Tusiogope kuingia gharama kuanza upya
mchakato wa kupata Katiba Mpya iwapo hakutapatikana maridhiano.
Tunatakiwa kujifunza kuanzia hapo.”
Kibodya alisema ni ngumu kwa Ukawa kuridhia mambo
yatakayopigiwa kura kwa sababu mengi waliyapinga na ndiyo ilikuwa sababu
ya umoja huo kususia vikao vya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu.
“Katiba ni ya nchi, si mali ya vyama vya siasa,
hivyo maridhiano ni muhimu. Kikubwa wakati wa utungaji wa Katiba ni
lazima yawepo maridhiano ya kisiasa. Rais Kikwete anatakiwa kutumia
hekima katika mkutano huo na washiriki wote kwa ujumla waondoe vichwani
mwao kwamba sisi ‘tumeshinda na wao wameshindwa’.
Alisema pamoja na mambo mengine, ni bora mchakato
wa kuandika Katiba Mpya ukachukua muda mrefu na gharama kubwa lakini
makundi yote yakakubaliana, tofauti na ilivyo sasa kwa baadhi ya watu
kwenda mahakamani na hii inaonyesha kuwa kuna tatizo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema, “Mkutano huo una
umuhimu mkubwa, ila ushauri wangu ni kuhakikisha kuwa pande zote
zinakubaliana na kuwa kitu kimoja.” Dk Makulilo alisema kama washiriki
wa mkutano huo watafikia mwafaka, makubaliano yao yanatakiwa kutoingilia
utaratibu wa Bunge la Katiba wa kupiga kura kupitisha kifungu kwa
kifungu, vinginevyo itakuwa ni kuingilia masuala ya kisheria.
“Katika hili napendekeza kuwa kitakachokubaliwa
kitumike katika hatua zinazoendelea za kupata Katiba Mpya. Unajua
mchakato ukiendelea kama ulivyo sasa bila mwafaka kupatikana Rasimu ya
Katiba inaweza kukataliwa na wananchi katika kura ya maoni. Kwa sasa
watu wanapinga mambo mengi yanayoendelea katika Bunge la Katiba,”
alisema Makulilo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali
Said alisema hatua ya Rais Kikwete kukutana na makundi yaliyosusia kikao
cha Bunge la Katiba ni mwafaka lakini kwanza Bunge hilo liahirishwe ili
kupisha mazungumzo hayo.
Awadh ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba alisema kitendo cha Bunge hilo kuendelea huku
kukiwa na kikao cha kutafuta usuluhishi ni sawa na mtu anayejenga nyumba
katika kiwanja chenye mgogoro.
“Kama umekubaliana na mwenzio kwamba tutakula
chakula baada ya kumaliza mazungumzo, si sahihi mmoja aendelee kula
mwingine akisubiri mazungumzo na ndicho wanachokifanya wajumbe wa Bunge
la Katiba,” alisema na kuongeza kuwa Bunge hilo limepoteza dira na
mwelekeo kutokana na viongozi wake kuanza kufanya kazi ya kukusanya
maoni ambayo ilikwishafanywa na tume, kitendo alichosema kinaonyesha
kuwa wameshindwa kuelewa mamlaka na majukumu ya chombo hicho. Naibu
Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui alisema licha ya
uamuzi wa Rais Kikwete kuchelewa, mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa
kwa vile ndiyo yatakayosaidia kupata Katiba Mpya yenye maridhiano.
Mazrui alisema CUF itashiriki katika mazungumzo hayo ambayo yanasimamiwa na TCD chini ya Mwenyekiti wake, John Cheyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai alisema
uamuzi wa Rais Kikwete ndiyo msimamo wa CCM uliofikiwa katika kikao cha
Kamati Kuu kuwa juhudi ziendelee kufanyika za kutafuta mwafaka ili Kundi
la Ukawa lirejee bungeni.
“Hatua hii ni muhimu, Katiba tunayoitafuta ina
manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano na lazima tupate
Katiba itakayosukuma mbele maendeleo ya wananchi wote,” alisema Vuai.
Katika hatua nyingine, Baadhi ya wananchi wilayani
Monduli wamekiomba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kufungua
kesi kuzuia uongozi wa Bunge la Katiba kuendelea kuvunja sheria kwa
kukusanya maoni ya makundi mbalimbali ya wananchi.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara
ulioandaliwa na LHRC, wananchi hao walisema kitendo hicho ni kinyume cha
Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinachoelezea kazi na
majukumu ya Bunge hilo.
“Kisheria, kazi na jukumu la kisheria la Bunge la
Katiba ni kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba baada ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi,” alisema
Thomas Mbwambo.
Mkazi mwingine, Eric Ngwijo alihoji uhalali wa
kura za maoni kwenye Katiba itakayopitishwa na Bunge Maalumu ambayo
viongozi wake wanavunja sheria kwa kupuuza maoni na mapendekezo ya
wananchi yaliyo katika rasimu.
Katika siku za karibuni, uongozi wa Bunge Maalumu
umekuwa ukikutana na kupokea mapendekezo na maoni kutoka makundi na watu
mbalimbali kwa kile unachodai ni kuingiza mawazo mapya yasiyokuwamo
kwenye rasimu.
Ofisa Mfawidhi wa LHRC Kanda ya Arusha, Shilinde
Ngalula aliwahimiza wananchi kushiriki mchakato wa Katiba Mpya na
kuwataka wajumbe wa Bunge hilo kuheshimu misingi ya mawazo na maoni ya
wananchi.
Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Fidelis Butahe, Peter Saramba na Zulfa Musa.
No comments
Post a Comment