Writen by
sadataley
1:38 PM
-
0
Comments
“Siyo sahihi kusema mkutano ulivunjika, bali kilichotokea ni wajumbe wa
pande zote mbili kutokubaliana, kisha mkutano ukaahirishwa kwa
kukubaliana kwamba siku yoyote tutarejea tena kwenye meza ya mazungumzo
ili kuendelea kujadiliana,”.PICHA|MAKTABA
Na Beatrice Moses, MwananchiDar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi amesema kuwa mkutano wa maridhiano kati ya wajumbe wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wale wa Chama cha Mapinduzi
(CCM), unaweza kuitishwa tena siku yoyote ili kurejea kwenye majadiliano
yao.
Jaji Mutungi aliyasema hayo kwenye mahojiano
maalumu na alieleza kushangazwa na kauli za watu wanaodai kuwa mkutano
huo ulivunjika, jambo ambalo alisema siyo kweli kwa sababu wajumbe wa
pande hizo mbili walimaliza mkutano huo kwa kukubali kutokubaliana hoja
zao.
“Siyo sahihi kusema mkutano ulivunjika, bali
kilichotokea ni wajumbe wa pande zote mbili kutokubaliana, kisha mkutano
ukaahirishwa kwa kukubaliana kwamba siku yoyote tutarejea tena kwenye
meza ya mazungumzo ili kuendelea kujadiliana,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema ingawa kwa upande wake alisikitika kwa
sababu alitamani maridhiano yafikiwe baina ya pande hizo kwenye kikao
hicho kilichofanyika siku nne kabla Bunge Maalumu la Katiba kuanza
mkutano wake wa pili.
Jaji Mtungi alisema kuwa kwa nafasi yake ya ulezi
wa vyama vya siasa, hajachoka, wala kukata tamaa kuendelea kusimamia
kikao hicho, ambacho kwa upande wa wajumbe wa Ukawa inavikutanisha vyama
vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF na upande mwingine CCM.
Awali, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alisema kuwa msimamo wao ni kutohudhuria vikao vya Bunge hilo labda
ikitokea miujiza kwa sababu kwa madai ya Ukawa ni lazima mjadala huo
ujikite kwenye Rasimu ya Katiba, ambayo imebeba mapendekezo ya wananchi
na kutaka wajumbe wenzao, hasa kutoka CCM, kuacha kujenga hoja kwa
kutumia kejeli, matusi na mizaha ambayo siyo rahisi wenzao kuyakubali.
Ukawa walisusia vikao vya Bunge la Katiba hilo
Aprili 16 wakipinga kubadilishwa Rasimu ya Katiba na wajumbe wa CCM kwa
maelezo kuwa ni kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Awali, Jaji Mutungi alizungumza na Mwanachi na
kueleza kuwa hatima ya Watanzania kupata Katiba Mpya itategemea busara
za viongozi wa vyama vya siasa.
“Ninavyoona mimi, hatima ya Watanzania ya kupata
Katiba Mpya itategemeana na busara za viongozi wetu wa vyama vya siasa
pekee na si kitu kingine.”
“Mambo siyo mepesi kama mnavyodhani, lakini yote
haya yanaweza kumalizika ikiwa busara itatumika... kwa viongozi wa vyama
vya siasa, kwa kila chama, kuweka mbele busara na utaifa kwanza na
mchakato utaendelea vizuri,” alisema Jaji Mutungi.
No comments
Post a Comment