Writen by
sadataley
1:33 PM
-
0
Comments
Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi.PICHA|MAKTABA
Na Beatrice Moses , MwananchiDar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa imeshindwa kutoa ripoti ya gharama za uchaguzi zilizotumiwa na
wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwamo ubunge na urais katika uchaguzi
mkuu uliopita mwaka 2010.
Ofisi hiyo ndiyo yenye jukumu la kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 na Sheria
ya Gharama za Uchaguzi namba 7 ya mwaka 2010 katika uchaguzi wowote.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi
alipohojiwa na gazeti hii kuhusu ripoti hiyo, ambayo huambatana na
mapendekezo ya adhabu kwa wahusika, alijibu kuwa bado wanaifanyia kazi.
“ Kuna changamoto ndogo ambazo tunakabiliana nazo,
ila kwa sasa siwezi kukutajia. Tunajitahidi kuifanyia kazi, ikikamilika
tunawajulisha,” alijibu Jaji Mutungi, lakini hakuwa tayari kutaja
changamoto hizo. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili,
umebaini kwamba ofisi hiyo haina wataalamu wa kutosha hasa wa hesabu
ambao wangeweza kufanya kazi hiyo kwa kiwango kinachotakiwa, hivyo kuwa
kikwazo. Takribani miaka minne imepita sasa, tangu ulipofanyika Uchaguzi
Mkuu, Oktoba 31 mwaka 2010, huku ikikumbukwa kuwa Machi 17 mwaka
huohuo, Rais Jakaya Kikwete alisaini Sheria ya Gharama za Uchaguzi
inayoagiza kuandaliwa na kutolewa kwa gharama zilizotumika na wagombea
nafasi mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi.
Machi mwaka huu, Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya
Siasa, Sisty Nyahoza wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze
alibainisha jinsi ofisi hiyo inavyowajibika kusimamia uchaguzi na sheria
hiyo kwa jumla. Nyahoza alisema kuwa katika kusimamia utekelezaji wa
Sheria ya Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatakiwa
kufuatilia na kutoa adhabu kwa vyama vya siasa vinavyojihusisha na
vitendo vilivyokatazwa.
Alisema kwamba vitendo hivyo ni pamoja na chama
ambacho wanachama au mashabiki wake wanajihusisha na vurugu, fujo na
uvunjifu wa amani wa aina yoyote.
“Vitendo vinavyokatazwa ni pamoja na chama ambacho
viongozi au wanachama wake wanatumia maneno ya matusi, kashfa na
uchochezi, kinatumia au mgombea wake anatumia mali za Serikali katika
kampeni na uchaguzi,” alisema.
“Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama
za Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina jukumu la kuweka
sawa uwanja wa ushindani katika siasa kwa kufuatilia na kupendekeza
adhabu inayopaswa kutolewa kwa chama cha siasa au mgombea anayejihusisha
na masuala yaliyokatazwa,”alielezea.
No comments
Post a Comment