Writen by
sadataley
11:54 AM
-
0
Comments
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.PICHA|MAKTABA
Na Elias Msuya, MwananchiDar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema CCM ndiyo iliyomsukuma kwenda
upinzani kama inavyofanya sasa kwa aliyekuwa kada wake, Mansour Yusuf
Himid.
Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika
Dar es Salaam hivi karibuni, Maalim Seif alisema CCM inajiundia
mashujaa watakaokuja kuipindua siku za usoni.
“Mimi sikuamua kuja upinzani, CCM ilinisukuma kama
anavyopitia Mansour sasa hivi. Kweli Mansour anapitia vilevile
nilivyopitia. Nilifukuzwa CCM, ilitafutwa tu sababu nikakamatwa na
kuwekwa ndani. Mansour naye hakutoka CCM, wamemfukuza,” alisema Maalim
Seif.
Mansour ambaye kabla ya kutimuliwa CCM alikuwa
waziri asiye na wizara maalumu na Mwakilishi wa Kiembesamaki, alivuliwa
uwaziri na baadaye uanachama kwa madai ya kukisaliti chama hicho.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF) alisema bado Mansour hajajiunga na upinzani, lakini
hutoa mchango wake wa mawazo katika majukwaa yake.
“Baada ya kufukuzwa akaona watu walio karibu na
msimamo wake ni CUF. Hajajiunga rasmi mpaka leo lakini huja kwenye
mikutano yetu kujieleza. Sasa wamemtia ndani, ipo siku watamtoa,”
alisema Maalim Seif na kuongeza:
“Lakini ‘they are making him a hero, they create
heroes themselves’ (wanamfanya awe shujaa, wanatengeneza mashujaa).
Nakumbuka Mwalimu Nyerere (Julius) aliwahi kuulizwa na Sauti ya
Ujerumani kwamba mambo gani anayojutia katika uongozi wake. Moja alisema
ni kuitambua Biafra na jambo la pili ni kuwafukuza kina Maalim Seif.”
Akifafanua zaidi jinsi alivyofukuzwa kutoka CCM,
Maalim Seif alisema Mwalimu Nyerere alifuata ushauri wa Idara ya Usalama
wa Taifa ya Zanzibar ambayo ilimtaka Seif na wenzake wafukuzwe mara
moja, huku idara hiyo upande wa Bara ikimwonya Mwalimu kutochukua hatua
hiyo.
“Kikao cha Dodoma kilichoitishwa, kilikwenda mpaka
saa sita usiku maana siku inayofuata Mwalimu alikuwa anasafiri na
ilikuwa ni lazima tufukuzwe tu. Utetezi tulioutoa, hata Job Lusinde na
marehemu Jamal walisema ‘mnawaonea tu vijana hawa, hawana kosa lolote’,”
alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya kufukuzwa alijiona
kuwa yuko huru zaidi, huku akifungua ukurasa mpya wa kuwa nje ya uongozi
wa Serikali.
“Kufukuzwa kwangu hakukuniuma, kwani nilijiona
nitakuwa huru kufanya mambo yangu na hasa nilipoona ninaungwa mkono na
Wazanzibari. Nilijiona kama nimepata baraka ya kuwa huru, wamenitesa,
lakini nikaona ni mapambano, hakuna kukata tamaa,” alisema.
Alipoulizwa iwapo ana mpango wa kurudi CCM siku za usoni, Maalim Seif alihoji:
“CCM? Hii ya kina Nape? Afadhali ile yetu sisi ya enzi hizo. Kwa
kweli haiwezekani. CCM ilikuwa ile ambayo Mwalimu ni Mwenyekiti, Kawawa
(Rashidi) ni Katibu Mkuu, kina Kingunge (Ngombale Mwiru), Moses Nnauye,
Salim Ahmed Salim, Alfred Tandau, ndiyo iliyokuwa sekretarieti. Siyo
CCM hii... Kwa nini hasa nijisumbue kurudi CCM wakati chama chetu
kinaendelea kuimarika?” alihoji.
Akanusha kumsaliti Jumbe
Kuhusu suala la kutofautiana na Rais wa Pili wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Aboud Jumbe ambapo Maalim Seif
anadaiwa kumsaliti katika Halmashauri Kuu ya CCM hadi akaondolewa kwenye
nafasi ya urais mwaka 1984, Maalim Seif amesema siyo kweli.
“Mimi sikupinga Serikali tatu. Wakati ule,
Wazanzibari katika chama tuligawanyika. Kuna wale wazee (waasisi)
wakijiita ‘Liberators’ kwa maana ndiyo walioleta mapinduzi, wakati huo
mimi ni kijana. Hata Aboud Jumbe alipoleta Katiba ya mwanzo waliipinga.
Lakini sisi vijana tukijiita ‘Front liners’ tulimuunga mkono,” alisema
na kuongeza:
“Hata katika kugombea nafasi za Nec kulikuwa na
makundi, haya yalikuwa yanagombana. Liberators walitaka sisi vijana
tusiiingie kwenye Nec. Hata hivyo, walikuta vijana wamekuwa wengi zaidi.
Hii iliwashtua Liberators.
“Wakahisi hawa vijana watachukua madaraka yao.
Walimlaumu sana Jumbe kutuingiza kwenye madaraka, sisi tulimsaidia Jumbe
kupitisha Katiba. Sasa fitina zikaanza, wanasema Waswahili papo kwa
papo.”
Kutokana na uhasama huo wa makundi, Maalim Seif
alisema kundi la Liberators lilizusha uongo kuwa amemsaliti Jumbe kwa
kukataa Serikali tatu:
“Baada ya kutokea uchaguzi mkuu wa chama, Jumbe
akaitisha kikao cha Unguja na Pemba mjini Dodoma. Katika hotuba yake
ndiyo ilitushtua kwani alizungumzia muungano na mgawanyo. Mwisho akasema
tunakwenda kwenye ‘revolutionary justice’ (mapinduzi ya haki). Hiyo
ilitushtua maana tulishaona watu wakipoteza maisha,” alisema na
kuongeza:
“Sasa mimi, Dk Salim Amour, Salim Ahmed Salim,
wakati huo ni wajumbe wa Nec, tutachukua majukumu kwa upande wa
Zanzibar. Tujue maana ya hii ‘revolutionary justice’. Tukaenda kwenye
sekretarieti ya chama tukalijadili.
“Sasa kwa sababu Liberators walishindwa kutuzuia,
ndipo walipokuja na suala la serikali tatu kutuengua. Nakumbuka hata
marehemu Sokoine (Edward) alimwambia Mwalimu, vijana hawa wakija
kupoteza maisha utawajibika. Sokoine alikuwa wazi sana, alikuwa Waziri
Mkuu mwenye maamuzi na anayejiamini na mwenye nguvu.”
Maalim Seif alisema walilazimika kumruka Jumbe kwa
kuwa hakuwashirikisha kikamilifu katika mpango wa mapinduzi aliyotaka
kuyafanya:
“Kama kweli Jumbe alikuwa anataka mamlaka zaidi ya Zanzibar,
sisi Wazanzibari wenzake kwa nini hakutuita walau tujadili na tuwe
sehemu ya madai hayo, ili tukija kwenye Nec tuwe pamoja? Anafanya chini
kwa chini? Kwa nini?”
Msimamo kuhusu Muungano
Maalim Seif amesisitiza msimamo wake katika muundo
wa muungano kuwa ni Serikali ya mkataba. Hata hivyo, licha ya muundo
huo kutoingizwa kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, anasema bado ameheshimu
uamuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Serikali ya Mkataba ni rahisi sana, Tanganyika
inakuwa na Serikali yake na Zanzibar Serikali yake. Kisha mnakaa pamoja
na kuangalia mambo gani mwendeshe pamoja. Jeshi, Polisi na mambo mengine
mnayoona kwa masilahi yenu kuyafanya pamoja,” alisema na kuongeza:
“Halafu siyo kuvunja muungano, haiwezekani leo
kusema muungano usiwepo kabisa. Miaka 50 hii siyo michache, watu
wamefanya mengi, wameshaoana sana. Lakini Wazanzibari leo wamebanwa,
koti la muungano limetubana sana. Sasa tunataka tupime ili tupate koti
ambalo haliwabani Tanganyika wala Zanzibar.”
No comments
Post a Comment