Writen by
sadataley
5:20 PM
-
0
Comments
Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda.PICHA|MAKTABA
Na Nuzulack Dausen, MwananchiDar es Salaam. Baadhi ya wafuasi wa Chama cha Tanzania
Democratic Alliance (Tadea), wameibuka na kuutuhumu uongozi wa chama
hicho kwa ‘kukivuruga na kukiuza’ kwa Mbunge wa Maswa Magharibi
(Chadema), John Shibuda.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari
Dar es Salaam jana kwa niaba ya wanachama wenzake, Joachim Mwingira
alisema uongozi umeshindwa kukisimamia chama hicho kikamilifu na tayari
umepanga kukibadili jina na kuhamisha makao makuu kwenda Mwanza.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tadea, John Chipaka
amekana kuuzwa kwa chama hicho na kuongeza kuwa hawatambui wanachama
hao, akiwamo Mwingira.
Kadhalika, Shibuda amesema hana mpango wa kukihama
Chadema kwenda chama kingine cha kisiasa licha ya kwamba vyama vingi
vinamuomba ajiunge navyo.
Mwingira aliyejiita mwasisi wa Tadea, alisema
hawamtaki Shibuda katika chama chao kwa kuwa amekuwa mvurugaji wa vyama
nchini na kwamba akishaharibu mambo ‘huteleza kama kambale.’
Katika maelezo yake, Chipaka alisema: “Hayo yote
ni mambo ya wahuni wa mtaani naomba wakuonyeshe uthibitisho kwamba Tadea
imeuzwa na ni kwa kiasi gani? Kuhusu kuhamisha makao makuu, alihoji..
“Kuna sheria gani ya vyama vya siasa inayotaka makao makuu yawe Dar es
Salaam pekee?”
Kuhusu suala la Shibuda, Chipaka alisema
mwanasiasa huyo ni Mtanzania kama wengine na anayo haki na uhuru wa
kuhamia chama chochote cha siasa anachopenda.
“Tadea ni Tadea. Suala la kubadilisha jina ni
tactics (mbinu) za kuimarisha chama, sasa hayo yanakujaje kuwa kwenye
vyombo vya habari. Ili chama kikue ni lazima kiwe na mbinu… waache
kuingilia mambo yetu ya ndani,” alisema Chipaka.
Kwa upande wake, Shibuda aliyeonekana kushtushwa
na taarifa hizo, alisema hatima yake ya siasa ipo ndani ya nafsi yake na
kwamba hakuna mtu atakayempangia.
“Sijatangaza kuondoka Chadema ila nilichosema ni
kwamba sitagombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama. Wao kama wana
ushahidi nimekinunua Tadea, wakupe hizo nyaraka na gharama
ujiridhishe,” alisema Shibuda.
Awali, Mwingira alisema asilimia kubwa ya wafuasi
wa Tadea hawautambui uongozi uliopo madarakani na kwamba wanaomba busara
za Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuwaruhusu wafanye
taratibu za kujiandaa na uchaguzi mkuu mwakani.
Alisema walishafungua kesi mahakamani kupinga
uongozi na kwamba wanaamini iwapo busara hizo zikifanyika, masuala ya
uongozi yatamalizwa nje ya Mahakama.
No comments
Post a Comment