Writen by
sadataley
3:56 PM
-
0
Comments
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak Abdulwakil akizungumza
jana kuhusu kufutwa kwa ajira 200 Uhamiaji. Kulia ni Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya jinai nchini (DCI), Isaya Mngulu. Picha na
Venance Nestory
Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani imefuta ajira 200 za
konstebo na koplo katika Idara ya Uhamiaji baada ya kubaini kuwa
kulikuwa na upendeleo katika usaili na sasa zitatangazwa upya na
kusimamiwa na wizara hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa
wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya
kamati maalumu ya kuchunguza ajira hizo kubaini wazi kwamba waliopewa
nafasi hizo hawakukidhi vigezo.
Abdulwakil alisema wizara imesikitishwa na udhaifu
huo baada ya kubainika wazi kwamba malalamiko yaliyotolewa na wananchi
na kusababisha wizara kuingilia kati na kufuta usaili wa kuitwa kwenye
ajira kwa watu 200 ulikuwa sahihi.
Alisema baada ya kubainika kwamba kweli kulikuwa
na upendeleo wa dhahiri kwani watahiniwa wenye sifa na waliopata alama
za juu wakati wa usaili hawakuitwa na kukiukwa kwa vigezo vya wazi,
ajira hizo zitatangazwa upya na kusimamiwa moja kwa moja na wizara na
siyo idara hiyo kama ilivyokuwa awali.
“Kamati hiyo iliyoanza kazi yake Agosti Mosi,
mwaka huu ilibaini kwamba hata kigezo cha umri, ambacho ni miaka 25 kwa
konstebo na miaka 30 kwa koplo hakikuzingatiwa kwani wenye umri zaidi ya
huo waliitwa kazini... “Lakini zaidi, baadhi ya wasailiwa walioitwa
kazini ni ndugu na jamaa wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji,” alisema.
Alieleza kwamba utaratibu mpya wa kuwapata watu
wanaostahili utatangazwa kupitia vyombo vya habari na mamlaka ya
usimamizi imerejeshwa kwenye wizara husika badala ya kuachiwa kwenye
idara husika.
Alisema pamoja na kwamba miongoni mwa udhaifu
uliobainika ni kwamba matangazo ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya
habari hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza
kidato cha nne na cha sita, lakini hata wale waliofanya vizuri katika
usaili hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalumu zilizotolewa.
Alisema ajira hizo zilizofutwa zinahusisha pia nafasi 28 zilizokuwa zimetangazwa kupitia Idara ya Uhamiaji Zanzibar.
Alisema si kosa kwa ndugu na jamaa wa watumishi wa
Idara ya Uhamiaji kuajiriwa katika nafasi hizo iwapo wanakidhi vigezo
vyote, lakini inapotokea kwamba hakuna msimamizi huru ni wazi kwamba
kunakuwa na upendeleo kama ilivyotokea na idara hiyo haichukui watumishi
kutoka Sekretarieti ya Ajira, kwa kuwa wanaohitajika ni askari.
Ajira hizo zilitangazwa Februari 17, mwaka huu na
watu 15,707 walijitokeza kuwania nafasi hizo 200, miongoni mwao,
waombaji 1,005 waliitwa kwenye usaili na 200 waliothibitishwa waliitwa
kazini.
Hata hivyo, baada ya tangazo la kuitwa kazini
malalamiko yaliibuka kupitia vyombo vya habari na baadhi ya mitandao ya
kijamii, kwamba baadhi ya walioitwa katika ajira hizo walikuwa ni
watoto, jamaa na ndugu wa maofisa wa Idara ya Uhamiaji.
Baada ya kuibuka kwa malalamiko hayo, wizara
iliingilia kati na kuunda kamati hiyo ya watu watano Julai 31, ambayo
ilipewa siku 10 kukamilisha kazi yake na kutoa matokeo.
No comments
Post a Comment