Sunday, September 14, 2014

Bunge Maalumu lilivyowavuruga Wanahabari


Ofisa Habari Bunge la Katiba, Owen Mwandumbya.PICHA|MAKTABA 
Na Habel Chidawali, MwananchiBunge Maalumu la Katiba linaeelekea ukingoni.Yapo mambo mengi yaliyofanywa kuhusu Mchakato wa Katiba ndani na nje ya Bunge hilo.

Mathalani katika shughuli za Bunge kulikuwa na idara na taasisi kadhaa ambazo bila ya uwepo wake kazi nzima isingeweza kufikia mahali hapa sasa.

Miongoni mwa idara hizo ni Habari na Itifaki ambayo kazi yake kubwa ndani ya bunge hilo ilikuwa ni kufanya shughuli zote za uratibu wa namna habari za bunge hilo zitakavyowafikia wananchi.

Vyombo mbalimbali vya habari vilituma wawakilishi wao katika Bunge hili ambao wamefanya kazi ya kupeleka kwa jamii kila kilichotokea ndani ya jengo hilo licha ya kuwa baadhi ya mambo watawala waliyapinga.
Oweni Mwandumbya ni mtumishi wa Bunge katika idara ya Habari na Itifaki ambaye wakati wote amekuwa karibu na vyombo vya habari na wanahabari katika kuhakikisha shughuli zao zinafanikiwa.

Akiwa ofisini kwake anazungumzia namna ambavyo kazi hiyo ilikuwa na msisimko mkubwa na jinsi jamii na wanahabari walivyomfanya akose usingizi wakati wote. Fuatilia mahojiano yake hayo na gazeti na gazeti hili:

Swali: Idara ya habari mmekuwa ni sehemu ya bunge hili, lakini muda mwingi hamuonekani kabisa na mnapoonekana ni pale ambapo mnabebeshwa lawama, nini mchango wenu?
Jibu: Ni kweli, unaweza kuona kama hatupo vile lakini ukweli ni kuwa bila ya idara hii pamoja na wanahabari wake, Watanzania walio wengi wasingeona kila kinachoendelea.

Swali: Kazi yenu ni nini hasa katika Bunge la Katiba?

Jibu: Kazi yetu ni kuratibu, kusimamia na kushughulikia masuala yote ya habari za Bunge la Katiba na kuhakikisha tunafikisha ujumbe kwa jamii.

Kazi nyingine ni kuweka mazingira ambayo yatamwezesha mwandishi wa habari wa Bunge la Katiba kufanya kazi yake kwa ufanisi bila wasiwasi.

Swali: Nani ni mwandishi wa habari za Bunge maalumu a Katiba, au kila mtu anaweza kuandika habari za Bunge hili?
Jibu: Hilo ni jambo muhimu la kuangalia, mwandishi wa habari za Bunge maalumu ni mtu ambaye amepimwa na kuonekana kuwa na weredi katika taaluma ya uandishi wa habari.

Ni mwandishi ambaye ameteuliwa na chombo chake na kuthibitishwa na Idara ya habari Maelezo na vyombo vingine maalumu ambavyo tunashirikiana navyo. Huyo ndiye anayestahili kupewa kitambulisho cha kufanya kazi ya Bunge maalumu.

Swali: Kuna tofauti yoyote kati ya mwandishi wa habari za Bunge Maalumu na mabunge mengine au kwa shughuli zingine za kawaida?

Jibu: Weledi na uzalendo ndiyo tofauti ya shughuli hii, walioitwa wengi wao walikuwa ni watu ambao hata ukiwaona unajua kabisa kuwa huyu ni mwandishi mzalendo.

Swali: Kuna unachoweza kujivunia katika kazi yako ndani ya Bunge hili maalumu.

Jibu: Yapo mengi, lakini kwa uchache ni kuwa tumefanikiwa kuifaya jamii iwe ni sehemu ya mchakato wa Bunge maalumu kwa kuwafikishia taarifa sahihi na kwa wakati.
Kingine ni pamoja na jinsi ambavyo tumekuwa sehemu muhimu ya kimbilio na wengi, nasema hivyo kwa kutambua kuwa kila tulipokuwa katika shughuli hii, watu wengi waliotaka kufikisha maoni yao walikimbilia kwa waandishi wa habari ili kutoa malalamiko yao au kero zao.

Swali: Kila kwenye mafanikio, kuna changamoto. Je, katika Bunge hili zipi changamoto mlizokutana nazo na kwa maoni yako unadhani changamoto hizo zilitokana na nini?

Jibu: Hakuna mahali kwenye mafanikio ambapo panaweza kukosa mapungufu, yapo baadhi ya mapungufu ambayo tulikutana nayo ni pale tulipopata habari za upotoshwaji kutoka kwa badhi yetu.

Swali: Umesema kuwa waandishi walioletwa katika Bunge hili walikuwa ni weledi, je upotoshwaji wa habari ulitokea wapi?

Jibu: Wapo ambao walikuja kwa weledi mkubwa na tuliwaamini lakini kadri mjadala ulivyokuwa unaendelea ni kama walipigwa na dhoruba na kujikuta wakifanya kazi ya kushabikia makundi fulani.

Jambo hilo lilijitokeza japo kwa uchache lakini tuliweza kukabiliana nalo kwa kuwaonya, kuzungumza nao na wakati mwingine kuwapeleka kwa katibu ili aweze kuzungumza nao na waliandika habari hizo kwa maana ya kufanya masahihisho.
Swali: Kwani hakukuwa na sheria za kuwabana watu wa aina hiyo na kutoa adhabu pale wanapokiuka?

Jibu: Sheria zilikuwepo, kumbuka kuna Kanuni ya 77 ya Bunge maalumu la Katiba ambao ilitungwa kwa makusudi kwa ajili ya watu hao. Ndani ya kanuni hiyo, inasema kuwa Katibu wa Bunge ana mamlaka ya kukifutia chombo au mwandishi wa habari ambaye atakiuka maadili ya kiuandishi ili asiripoti habari za bunge maalumu.

Mwandumvya anasimulia kuwa hali kama hizo zilipojitokeza, walitumia busara zaidi kuliko sheria na kanuni za Bunge la Katiba hali iliyofanya mchakato uendelee kuwa salama kwa waandishi wa habari.

Jingine analosikitikia ni namna ambavyo kumeibuka a vyombo vya habari visivyo na uwakilishi kwa Bunge maalumu ambavyo kila wakati vinaripoti habari za Bunge kwa upotoshwaji mkubwa kwa kuwa kazi yao ni kuangalia kwenye luninga tu.

Akizungumzia tofauti ya Bunge hili na Bunge la Muungano, anasema iko kubwa kwani Bunge la Katiba linaangalia kwa sehemu kubwa na mataifa mengi ya nje na Watanzania wenyewe wakati Bunge la Jamhuri ni la kawaidalinaloshughulikia masuala ya utendaji ya kila siku.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment