Writen by
sadataley
12:30 AM
-
0
Comments
Tumwogope Mungu, kwa matendo yetu mabaya, Tuogope
kuwatendea ndugu zetu yale tusiyopenda kutendewa sisi. Tumwogope Mungu,
tunapopokea sadaka na zaka nzito nzito kutoka mikononi mwa wanasiasa,
bila kuuliza wala kuhoji.
Tumwogope Mungu, tunapowakumbatia wanasiasa wenye
sifa za ufisadi na kuwaalika kuendesha harambee za kujenga misikiti na
makanisa.
Tumwogope Mungu, tunaposamehewa kutoa ushuru na
badala ya kuwahudumia wanyonge na maskini, tunajitenga na jamii na
kuishi maisha kifahari.
Tumwogope Mungu, tunapokula na kusaza, wakati
wengine wanakufa kwa njaa. Tumwogope Mungu, tunapoziingilia familia na
kuzisambaratisha. Tumwogope Mungu, tunapozaa watoto na kuwatelekeza
kwenye mitaa ya miji.
Tumwogope Mungu, pale tunaposhughulikia afya zetu
kwenye hospitali nzuri na kuwaacha wanyonge kufa kwa magonjwa
yanayotibika. Orodha ni ndefu! Ni lazima kumwogopa Mungu, kwa matendo
yetu yote mabaya.
Kwa viongozi wetu wa dini za Kikristu, ujumbe huu
unaweza kuwasaidia kutafakari zaidi: “… Nendeni katika moto wa milele
aliotayarishiwa shetani na malaika wake. Maana nilikuwa na njaa nanyi
hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu hamkunipa maji; nilikuwa mgeni
hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama…
Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa
hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi” (Mathayo 25: 41- 46).
Yesu, alizungumzia mambo yanayotendeka kila siku
katika jamii, mambo ambayo yanawatenga watu na Mungu wao. Hivyo orodha
hii inaweza kurefushwa:
“Mlinibagua kufuatana na rangi yangu ya mwili,
kabila langu na dini yangu, mlininyanyasa, hamkunisikiliza, hamkunionea
huruma nilipolala mitaani, hamkunipatia ushauri mzuri mume wangu
alipoanza kutembea nje ya ndoa na kuambukizwa virusi vya Ukimwi.
Mlinibagua, mlinibaka, mlinitomasa na kuninyanyasa kijinsia...
n.k.”Orodha ni ndefu. Hoja ni kwamba ni lazima kumwogopa Mungu, kwa
matendo yetu yote mabaya.
Yule anayewanyanyasa wanawake na kuwanyima nafasi
ya uongozi katika kanisa na nafasi ya kufanya uamuzi muhimu katika jamii
kama vile ndoa na familia, kuzaa watoto wengi au kuzaa kwa mpango,
kutoa mimba au kulinda uhai kwa kupoteza uhai.
Mfano, mwanamke mwenye matatizo kwenye kizazi,
ambaye kama angetoa mimba, angeponyesha maisha yake), kuhusu malezi
n.k., ni lazima amwogope Mungu, maana kuwabagua na kuwanyanyasa wanawake
ni kumbagua Mungu Mwenyewe.
Tunafundishwa kwamba sote tumeumbwa kwa mfano wa
Mungu na kwamba binadamu wote ni sawa. Bahati nzuri Katiba yetu
inakubaliana na kitu hiki.
Yule anayewabagua watu wa dini nyingine, ni lazima amwogope
Mungu, maana sisi sote ni watoto wa Mungu. Ukweli unaotuzunguka sasa
hivi ni kwamba wapo wanajiona wana haki zaidi ya wengine.
Wakristu wanagawanyika katika madhehebu ambayo
kila moja linajiona kuwa na haki zaidi ya mengine. Dini zinageuka kuwa
kikwazo cha ushirikiano, udugu kama vile ndoa n.k., wakati mwingine hata
viongozi wa serikali wanachaguliwa si kwa sifa bali kwa kufuata dini
zao.
Habari njema inakuja kwa maskini, wafungwa na
wanaoonewa, si kwa matajiri na wenye madaraka. Ili ujumbe huu uwe na
maana, Yesu, mwenyewe alijitokeza miongoni mwa maskini na wanaoonewa.
Alizaliwa katika umaskini na kukulia katika
umaskini. Enzi zake kulikuwa na matajiri wenye majumba ya kifahari,
lakini hakuyachagua! Aliishi na maskini.
Mitume wake wote walikuwa ni watu maskini.
Aliwaponya wagonjwa, waliwafufua wafu na kuwapatia uzima mpya, uzima
tele. Wenye njaa aliwashibisha chakula cha mwili na roho, wenye kiu
aliwapatia maji ya uzima. Alifanya miujiza mingi bure bila kudai ujira.
Ili ujumbe wa viongozi wetu wa dini na hasa
Wakristu uwe na maana yoyote ile ni lazima wajiulize wamesimama upande
gani? Kama zilivyokuwa enzi za Yesu, leo hii kuna matajiri na maskini,
kuna majumba ya kifahari na kuna vibanda ambavyo ni sawa na zizi la
ng’ombe alikozaliwa Yesu.
Viongozi wetu wa dini wanaishi kwenye majumba ya
kifahari au kwenye vibanda? Wanapanda daladala au magari ya kifahari?
Je, wako upande wa maskini na wanaoonewa au upande wa matajiri na wenye
madaraka.Je, wanawaponya wagonjwa? Wenye njaa wanawapatia chakula? Wenye
kiu wanawapatia maji ya kunywa? Je, wanafanya miujiza bila ya kudai
ujira?
Viongozi wetu wa dini na hasa Wakristu,
wanapotukumbusha kumwogopa Mungu, ni bora wao wakatafakari ujumbe wa
Yesu kwanza. Je, wao wanamwogopa Mungu? Je, wao wanashiriki kiasi gani
kuchangia hali hii ya watu kuishi bila kumwogopa Mungu.
Kwanini watu waamue kuuza haki yao ya kupiga kura?
Kwanini watu waamue kumchagua kiongozi si kufuata sifa zake bali
wafuate kabila, dini, pesa, pilau na kanga wanazozipata wakati wa
kampeni?
No comments
Post a Comment