Friday, September 12, 2014

Usajili jina la biashara sasa warahisishwa


 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Mchakato wa kusajili jina la biashara kwa sasa utakamilika ndani ya saa nane za kazi badala ya zaidi ya siku saba kama awali.

Hayo yalisemwa jijini hapa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ambaye pia ni Msajili wa Kampuni, Frank Kanyusi.

Alisema kazi hiyo inayofanyika kielektroniki inalenga kuimarisha mazingira ya biashara nchini.

Alisema wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wamebuni mfumo utakaowawezesha watu kusajili jina la biashara kwa urahisi na ufanisi zaidi. “Watu wanaosajili jina la biashara wameongezeka maradufu na malalamiko yamepungua kwa kiwango kikubwa,” alisema.

Akizungumzia faida za mfumo huo mpya, alisema utawawezesha watu wengi zaidi kuwa na majina rasmi ya biashara na hivyo kutambulika kwa taasisi za fedha na kupata mikopo. Pia alisema mfumo huo utaiwezesha Serikali kuwafahamu watu waliosajiliwa kisheria na hivyo kurahisisha ukusanyaji kodi.
Ofisa huyo aliwataka wananchi wasidanganywe na mtu kuhusu utaratibu wa kusajili jina la kampuni kwa kuwa hakuna mtu wa kati atakayehusika.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment