Friday, July 10, 2015

JK avunja Bunge, ataja mafanikio ya miaka 10

Rais Jakaya Kikwete amelihutubia Bunge la 10 kwa mara ya mwisho, akijikita katika takwimu zinazoonyesha mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Nne imeyapata tangu alipoingia Ikulu mwaka 2005, lakini akakiri kutofanikiwa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Hali iliyokuwa mwaka 2010 wakati alipohutubia Bunge hilo kwa mara ya kwanza, ndiyo iliyojirudia jana baada ya wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao na kuwaacha wapinzani wachache. Rais Kikwete, ambaye alihutubia kwa saa 2.20 alitangaza kulivunja Bunge la 10 lakini akasema litavunjwa rasmi Agosti 20, akieleza kuwa shughuli ya jana ilikuwa kama “kitchen party au send off”. Katika hotuba yake, Rais Kikwete alimmwagia sifa Spika Anne Makinda, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi mbalimbali wa Serikali, wananchi na chama chake kwa kumuamini, huku akisisitiza kuwa anaondoka madarakani na kuiacha nchi ikiwa salama. Huku akishangiliwa na wabunge, Rais Kikwete alieleza kuwa Serikali yake ilipata mafanikio katika utawala bora, uhuru wa habari, vita dhidi ya rushwa, kukua kwa mapato ya Serikali, maadili ya viongozi, mihimili ya Serikali, uanzishwaji wa wilaya mpya, nyongeza ya mishahara, mifugo na uvuvi. Ushiriki wa wanawake katika uongozi, kukuza uchumi, utalii, viwanda, madini, umeme, uchukuzi, huduma za kibenki, michezo, masilahi ya wafanyakazi, burudani, ajira, utamaduni, Muungano, amani na umoja ni masuala mengine ambayo mkuu huyo wa nchi ameeleza yalikuwa na mafanikio. “Desemba 30, 2005 nilipozindua Bunge la Tisa nilielezea mtazamo wangu kuhusu nchi yetu na kutaja majukumu ya msingi na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nne. Nilisema tutatekeleza wajibu wetu na vipaumbele hivyo kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya,” alisema. Alifafanua kuwa Julai 16, 2010 wakati wa kuvunja Bunge la Tisa alieleza mafanikio yaliyopatikana na changamoto zake na Novemba mwaka huohuo wakati akilizindua Bunge la 10, aliahidi kutekeleza vipaumbele vya Serikali kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi, jambo ambalo alisema amelifanya kwa kiwango kikubwa. Alisema marais waliopita, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi walifanya mambo mengi mazuri lakini hawakumaliza yote na kusisitiza kuwa kila jambo lina changamoto zake. “Hata Baba wa Taifa hakumaliza yote na mimi ninamuachia Rais ajaye ayamalize yale ambayo mimi sikuyamaliza,” alisema Rais Kikwete. Akizungumzia sekta ya kilimo, Rais alisema licha ya juhudi kubwa iliyofanywa na Serikali, bado kuna changamoto katika upatikanaji wa masoko ya uhakika na bei nzuri kwa mazao ya wakulima. “Pia kuna tatizo la upungufu wa maghala ya kuhifadhia mazao. Jitihada zinaendelea kupata mkopo au wabia wa kujenga maghala ya kisasa nchi nzima. Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushiriki ilianzishwa ili kutatua tatizo la masoko,” alisema. “Tumeanza maandalizi ya Commodity Market Exchange (soko la bidhaa) kwa nia hiyohiyo. Naamini misingi mizuri tuliyoijenga pamoja na kuenea kwa saccos na kuanza kwa Benki ya Kilimo, tutatoa mchango mkubwa katika kuongeza kasi ya mapinduzi ya kilimo.” Alisema lengo la kuendeleza sekta ya kilimo ilikuwa ni kuongeza tija ili uzalishaji uongezeke, wakulima wapate mavuno mengi, masoko ya uhakika yawepo na bei iwe nzuri ili mapato yao yaongezeke na umaskini uwapungukie. Alisema kwa kutambua hilo, mwaka 2006 Serikali ilisaini programu ya miaka saba ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP), kwamba katika programu hiyo matatizo yanayofanya tija na uzalishaji katika kilimo kuwa mdogo yalitambuliwa na kutengenezewa mpango wa kuyatatua. Alitaja mipango mingine ya kuongeza msukumo katika kuleta mageuzi ya kilimo iliyoanzishwa ni Kilimo Kwanza, Mpango wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo (TAFSIP), Sera ya Umwagiliaji na Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika. Alisema katika kuhakikisha kuwa kilimo kinaboreshwa, Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya kilimo kutoka Sh233.3 bilioni mwaka 2005/06 hadi Sh1,084.7 bilioni mwaka 2014/15. “Kuongezwa kwa bajeti kumewezesha fedha za ruzuku ya mbolea na pembejeo kuongezeka kutoka Sh7.5 bilioni mwaka 2005/06 hadi Sh299.3 bilioni mwaka 2013/14,” alisema. Alisema matrekta makubwa na madogo yameongezeka kutoka 7,491 mwaka 2005 hadi 16,412 mwaka 2014. “Kwa sababu hiyo matumizi ya jembe la mkono yamepungua kutoka asilimia 70 hadi asilimia 62. Tumeongeza maofisa ugani kutoka 3,379 mwaka 2005 hadi 7,974 mwaka 2014,” alisema. Katika usafiri wa anga, Rais Kikwete alisema Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuwekeza kwenye ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege nchini, licha ya kushindwa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (TTCL). “Hatua hiyo imesaidia sana ongezeko kubwa la safari za ndege na abiria nchini. Safari za ndege kuja nchini zimeongezeka kutoka safari 78 mwaka 2005 zilizokuwa zinatolewa na kampuni 29 za usafiri wa ndege, hadi safari 175 zinazotolewa na kampuni 55 mwaka 2014,” alisema. “Jambo ambalo hatukuweza kufanikiwa ni lile la kufufua ATCL. Tumefanikiwa kulifanya lisife lakini hatukuweza kulihuisha lirejee hata kwenye ile hali yake ya zamani. “Fikra na mawazo kuhusu mkakati wa kulijenga upya shirika hilo ipo. Kwa sasa menejimenti imepewa jukumu la kuandaa mpango wa biashara unaoeleweka na unaokopesheka, kisha Serikali itaona namna ya kulisaidia.” Chanzo:mwananchi.co.tz
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment