Writen by
sadataley
6:10 AM
-
0
Comments
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu (39) amesema anayo nia na uwezo wa kumuangusha katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu, mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini anayemaliza muda wake Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Msambatavangu aliyasema hayo alipokuwa akitangaza nia yake ya kugombea Ubunge katika jimbo hilo la Iringa.
“Tunajianda kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao tukiwa wamoja na niwahakishieni mimi ni mmoja kati ya wana CCM wenye nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Iringa Mjini,” alisema.
“Sijajua makada gani wengine watajitokeza; wenye uwezo wa kusema ni nani ni CCM wenyewe na wananchi wa jimbo hili. Kwa mimi kutangaza nia na kujitoa nina hakika na ninafahamu nina uwezo wa kupeperusha bendera na kurudi na ushindi, sitakiletea aibu Chama cha Mapinduzi pamoja na kwamba nipo tayari kumuunga mkono mgombea atakayeteuliwa,” alisema.
Alitaja kipaumbele chake cha kwanza endapo CCM itampa ridhaa ya kuwania nafasi hiyo kuwa ni elimu na katika sekta hiyo atakahikisha miundombinu yake inaboreshwa ili iwe ya kisasa.
“Nitahakikisha kunawepo na ustawi wa elimu, shule bora zenye nidhamu ili Iringa iingie kwenye ushindani wa juu kitaifa. Tutajiimarisha kujenga mabweni katika shule zetu ili watoto hasa wa kike wawe jirani na shule,” alisema.
Alisema katika kuboresha ustawi wa sekta hiyo atahakikisha vijana wengi wa shule za msingi na sekondari za mjini Iringa wananufaika kwa uwepo wa vyuo vikuu vinne vya mjini hapa kwa kutengeneza ushirikiano utakaosaidia vijana wengi kujiunga na elimu ya juu.
Alitaja vipaumbele vyake vingine kuwa ni kusaidia kuboresha shughuli za kijasiriamali na kuufanya mji wa Iringa kuwa wa kibiashara ili kuongeza ajira kwa vijana wakiwemo wale wanaomaliza vyuo vikuu.
“Hiyo itakwenda sambamba na kutenga maeneo ya biashara kwa vijana; tutakaa nao, kufahamu mahitaji yao na kuyafanyia kazi, lakini nitaziangalia na kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali katika sekta zingine ikiwemo ya afya, miundombinu, michezo, wafanyakazi katika sekta binafsi na umma” alisema.
Alisema endapo atachaguliwa atafanya ziara na kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii katika kata zote za mji wa Iringa, kuyachukua matatizo yao na kuyayafanyia kazi kwa kuzingatia majukumu ya kibunge na nafasi yake katika jamii.
Akizungumzia nguvu ya Chadema mjini Iringa, Msambatavangu alisema; “pamoja na CCM kuwa wapinzani katika jimbo la Iringa Mjini, bado tuna nguvu ya kutosha kisiasa na ndio maana tulipata viti vingi vya serikali za mitaa ikilinganishwa na Chadema walioko madarakani kwa mwaka wa tano sasa.”
Katika uchaguzi huo, CCM ilipata viti 126 huku Chadema wakipata viti 64 na CUF wakipata kiti kimoja.
Kama atatimiza azma yake hiyo, Msambatavangu, msomi mwenye shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara, atakuwa anaingia kwa mara ya pili katika kinyang’anyiro hicho huku ikikumbwa kwamba katika kura za maoni za chama hicho za mwaka 2010 zilizoshirikisha wagombea 12 alishika nafasi ya nne baada ya kujipatia kura 916, nyuma ya Frederick Mwakalebela aliyepata kura 3,897, Monica Mbega 2,989 na Dk Yahaya Msigwa aliyepata kura 1,217.
Wengine walioshiriki kinyanganyiro cha 2010 na kura zao kwenye mabano ni Fadhili Ngajilo (536), Addo Mwasongwe (383), Zuberi Mwachula (324), Benigus Mpete (242), Thomas Kimata (201), Chelestino Mofuga (192) na Dk Raphael Kalinga (169).
Chanzo:Frankleonard Info
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments
Post a Comment