Writen by
sadataley
12:13 PM
-
0
Comments
Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli
MKUTANO Mkuu Maalumu wa CCM utaleta mtikisiko ndani ya chama na
umefanya wajumbe kuwa matumbo moto kutokana na ajenda kubwa ya
kukifanyia mageuzi, kwa kubadilisha Katiba yake na kupunguza wajumbe wa
mikutano ya chama.
Mtikisiko uliopo unatokana na chama hicho, kuitisha mkutano huo
kubadilisha Katiba yake ya mwaka 1977 ambayo ilifanyiwa marekebisho yake
kwa mara ya mwisho mwaka 2012. Haijafanyiwa marekebisho mengine kwa
zaidi ya miaka mitano.
Matumbo moto ya wajumbe yanatokana na azma ya mkutano huo, utakaofanyika
katika ukumbi wa Dodoma Conventional Centre mjini hapa, kupunguza zaidi
ya nusu ya idadi ya wajumbe waliokuwa wakihudhuria mikutano ya Kamati
Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mkutano Mkuu wa chama.
Mkutano Mkuu huo utakaoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John
Magufuli utafanyika Jumapili Machi 12, mwaka huu, ukitanguliwa na kikao
cha Kamati Kuu (CC) kitakachofanyika Machi 10 na NEC itafanyika Machi
11, mwaka huu.
HabariLeo ilitembelea Makao Makuu ya Chama mjini hapa, ambapo pilika
pilika za kupamba zilikuwa zikiendelea huku Chipukizi, wakiweka bendera
na baadhi ya wajumbe wa vikao hiyo kutoka mikoa 31 ya Tanzania, walikuwa
wakibadilisha mawazo ndani na nje ya ofisi.
Wakati upambaji ukiendelea makao makuu, pia maandalizi yalikuwa
yamepamba moto katika ukumbi wa Dodoma Conventional Centre,
utakapofanyikia mkutano huo, kwa kugawa na kupanga maeneo maalumu ya
kukaa viongozi, wajumbe, wageni waalikwa na waandishi na hata maeneo ya
maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali, zitakazokuwapo eneo hilo.
Taarifa iliyotolewa awali na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rodrick
Mpogolo, ilisema mkutano huo unafanyika kufuatia mageuzi makubwa
yanayofanyika ndani ya Chama, ambayo yalihitaji kufanyika marekebisho ya
kanuni na Katiba ya chama.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa, Mpogolo alisema,
mkutano huo una umuhimu mkubwa kutokana na ajenda ya kuangalia ratiba ya
uchaguzi ndani ya chama mwaka huu, lakini hasa ya kuzifanyia
marekebisho sheria mama za chama hicho kikongwe zaidi na imara barani
Afrika.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphey Polepole aliahidi atazungumza
kesho kuhusu mkutano huo wa kihistoria. Alidokeza kuwa ajenda kubwa ya
mkutano huo ni kurekebisha sheria mama ya chama hicho.
Marekebisho yatakayofanywa na mkutano huo mkuu maalumu kuhusu Katiba ya
CCM, yatafuta, kurekebisha au kuongeza kwenye marekebisho ya awali
yaliyofanyika ndani ya chama tangu mwaka 1977 hadi 2012.
Katika mazungumzo, mwandishi mkongwe wa chama, Charles Charles alisema
mkutano huo ni muhimu zaidi kuliko uliofanyika mwaka jana, ambao ulikuwa
rasmi kwa ajili ya kupokezana kijiti cha kuongoza chama kutoka kwa
mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete kwenda kwa mwenyekiti wa sasa, Rais
John Magufuli.
“Pia mkutano huu ni muhimu zaidi hata kuliko wa mwaka juzi, ambao chama
kilikuwa kikitafuta mgombea ndani ya chama, ambapo kulikuwa na misuguano
mingi kwani kwa mara ya kwanza chama kilikuwa na wagombea zaidi ya 30
wa nafasi hiyo,” alisema.
Mchujo wa awali wa urais, ulishirikisha wagombea urais 43, ambapo wengi
walienguliwa na wakabaki watano. Wengine wawili nao walienguliwa katika
mchujo wa pili. Mchujo wa tatu ulishirikisha majina matatu, yaliyopigiwa
kura kwenye mkutano mkuu, ambapo Rais Magufuli alishinda kwa kishindo.
Wagombea wawili kura zao hazikutosha. Charles alisema mkutano huo wa
wiki hii, umeibua hamasa kubwa na kuleta matumbo moto kwa wajumbe
kutokana na mkakati wa chama wa kupunguza idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu
kutoka 34 hadi 24, Halmashauri Kuu kutoka 338 hadi 234 na wajumbe wa
Mkutano Mkuu kutoka 3,800 hadi takribani 1,800.
Alisema, kupunguzwa kwa idadi ya wajumbe ambao walikuwa wajumbe wa
mikutano hiyo, ndiko kunaibua hofu miongoni mwao, hasa pale ambapo kwa
mfano kwenye nafasi hiyo walikuwa wajumbe saba, sasa wanatakiwa
kupunguzwa na kubaki mmoja.
“Kupunguza idadi ya wajumbe katika mkutano huo, kunawafanya baadhi ya
wajumbe kuwa na matumbo moto kutokana na kwamba watapoteza vyeo, hasa
waliokuwa wakishiriki viwili au zaidi na kwamba watabakia na cheo kimoja
tu,” alisema.
Mwandishi huyo mkongwe alisema, baadhi ya wajumbe walikuwa wakitumia
vyeo vingi kama kinga. Walikuwa hawajabadili kutokana na kuwa na vyeo
ambavyo wanavisimamia, hivyo kuwa vigumu kuwawajibisha.
Panga hilo la chama la kupunguza wajumbe, litaenda sambamba na kufyeka
idadi kubwa ya vikao katika ngazi zote za shina, tawi, kata, jimbo,
wilaya, mkoa hadi taifa. Lakini, pia panga hilo litagusa jumuiya za
chama za Vijana, Wanawake na Wazazi.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli akiwa na mkewe, Mama Janeth, aliwasili
mjini hapa Machi 7, mwaka huu. Mwishoni mwa mwaka jana, alisema chama
hicho kimefanya mageuzi na kinalenga kupunguza wajumbe. Aliahidi
angeitisha Mkutano Mkuu Maalumu ili kupunguza wajumbe na nyadhifa zao.
Mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kufanywa CCM ni : Wajumbe wa NEC ambao
sasa wapo 388, watapunguzwa hadi wajumbe 158, sawa na asilimia 40.
Vikao vya kawaida vya NEC navyo sasa vitafanyika kila baada ya miezi
sita, badala ya miezi minne, ilivyo sasa.
Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, nao watafyekwa kutoka 34 waliopo sasa hadi
24 tu. Kwa upande wa vyeo, inapendekezwa kuwa kuanzia sasa kila
mwanachama, atatakiwa kushika cheo kimoja tu; au nafasi moja tu ya
uongozi wa kazi za muda wote.
Kazi hizo ni Mwenyekiti wa tawi, kijiji au mtaa, kata, jimbo, wilaya na
mkoa, makatibu wa Halmashauri Kuu wa ngazi zote, Mbunge, Mwakilishi na
Diwani.
Mapendekezo mengine ni kufuta vyeo ambavyo havijatamkwa kwenye Katiba ya
CCM na jumuiya zake ; na mfano wa vyeo hivyo ni Mwenyekiti wa wenyeviti
wa CCM, makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Washauri wa Umoja
wa Wanawake (UWT) na Walezi wa Jumuiya ya Wazazi.
Chanzo:Muungwana Blog

No comments
Post a Comment