Writen by
sadataley
2:08 PM
-
0
Comments
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
inatararajia kuanza upasuaji wa kupandikiza Moyo kwa wagonjwa wenye
matatizo ya moyo nchini.
Mkurugenzi wa Upasuaji na Daktari Bingwa
wa Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu Dkt. Bashir Nyangasa ameyasema
hayo leo Jijini, Dar es Salaam alipokuwa akiongea na vyombo vya habari
kuhusu malengo ya Taasisi hiyo.
“Tuko katika maandalizi ya kuandaa
mapendekezo kwa ajili ya kupeleka Bungeni ili Bunge lilidhie na
kupitisha sheria itakayoruhusu mtu kuandika wosia wa viungo vyake
kutumika mara baada ya kufariki, ikiwemo moyo, figo na viungo vingine,”
alifafanua Dkt. Nyangasa.
Aliendelea kwa kusema kuwa, umefika
wakati kwa watanzania kujiwekea utaratibu wa kuacha wosia wa kutumika
kwa viungo vyao mara baada ya kufariki kwa ajili ya kuhifadhiwa katika
benki za viungo ili viweze kutumika na watu ambao wanauhitaji.
Aidha Dkt. Nyangasa amesema hospitali ya
Apolo Bangalole ya India na hospitali nyingine za kimataifa za magonjwa
ya moyo kwa sasa zimehamia JKCI kutokana na huduma pamoja na vifaa
vinavyopatikana katika hospitali hizo vinapatikana katika Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Huduma
za Tiba, Daktari Bingwa wa Wagonjwa wa Moyo Dkt. Tulizo Shemu amesema
kwa mwaka 2016 Taasisi imefanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa 973, kati
ya wagonjwa hao 620 walipatiwa matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua
kwa kupitia mishipa ya damu (Catheterization) na wagonjwa 353
walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua.
Vilevile amesema kuwa kwa mwaka huu wa
2017 Taasisi hiyo imejipanga kufanya upasuaji wa kupasua kifua kwa
wagonjwa 700 na wagonjwa wengine 1000 watafanyiwa operesheni bila ya
kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa ‘Catheterization’.
Taasisi hiyo inategemea kuwa na kambi
maalum ya matibabu ya moyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Open Heart
International ya nchini Australia kuanzia Machi 10, 2017 ambapo wagonjwa
25 wakiwemo watoto 15 na watu wazima 10 watafanyiwa upasuaji.
Wananchi wameombwa kujitokeza kuchangia damu kutokana na uhitaji wa damu nyingi katika upasuaji huo.
No comments
Post a Comment