Writen by
sadataley
2:12 PM
-
0
Comments
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania
Jenerali Venance Mabeyo amefanya ziara ya kikazi Mkoani Kagera kukagua
maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kabyaile Wilayani Missenyi
kinachojengwa upya na Jeshi la Wananchi Tanzania mara baada ya
kuathiriwa na Tetemeko la Ardhi lililotokea Mwezi Septemba mwaka jana.
Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo alifanya
ziara hiyo Machi 2, 2017 na lengo kuu ilikuwa ni kuona maendeleo ya
ujenzi wa kituo hicho mara baada muda alioutoa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kuisha mwishoni mwa mwezi
Februari mwaka huu 2017.
Rais Magufuli alipofanya ziara Mkoani
Kagera Januari 1, 2017 alitembelea eneo la Kabyaile Wilayani Missenyi na
kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya na kuagiza kuwa
ujenzi huo uwe umekamilika ifikapo Mwisho mwa mwezi Februari 2017.
Mara baada ya kukagua maendeleo ya
ujenzi huo Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo akiongea na viongozi wa mkoa
na wananchi waliofika kumuona kituoni hapo alisema ameridhishwa na hatua
iliyofikiwa katika ujenzi huo, pia alishukuru upanuzi wa majengo kuwa
ni manufaa kwa wananchi wa Kabyaile na Wilaya ya Missenyi kwa ujumla.
Pia aliwashukuru wananchi kwa
ushirikiano wao na kikosi cha Jeshi la Wananchi Tanzania kinachojenga
kituo hicho kuwa kikosi hicho kinafanya kazi katika hali ya utulivu na
amani na wananchi wenyeji, aidha aliwaomba wananchi kuwaona wananjeshi
kama raia wengine na kuendelea kuwapa ushirikiano kwani wanatokana na
Watanzania wenyewe.
Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo baada ya
kukagua ujenzi na kupata maelezo ya kina alisema kuwa muda alioutoa
Rais Magufuli wa hadi mwishoni mwa Mwezi Februari 2017 ujenzi haukuweza
kukamilika kwasababu kuna kazi zingine za ziada ambazo zilijitokeza na
kushindwa kukamilisha kituo hicho kwa muda uliotolewa.
?Kwa kazi alizoelekeza Rais Magufuli
tayari zipo katika hatua za mwisho kabisa za umaliziaji, pia na kazi
zilizoongezeka zipo katika hatua nzuri ya ujenzi na kufikia mwishoni mwa
mwezi Machi 2017 kazi zote zitakuwa zimekamilika zote? Aliwaeleza
wananchi Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Majeshi ya
Tanzania Jenerali Mabeyo alitembelea pia ujenzi wa Shule ya Sekondari
Omumwani Katika Manispaa ya Bukoba kunakojengwa vyumba viwili vya
mabweni na Kikosi cha Jeshi la Wananchi Tanzania, aidha alimalizia ziara
yake katika Shule ya Sekondari Ihungo na kukagua ujenzi mpya wa shule
hiyo iliyoharibiwa na tetemeko pia mwezi Septemba Mwaka jana 2016.
Chanzo:Mjengwa Blog
No comments
Post a Comment