Thursday, March 30, 2017

Ripoti yabaini madudu elimu ya msingi Kilombero

Ripoti ya ufuatiliaji wa mgawanyo na matumizi ya rasilimali za umma katika sekta ya elimu ya msingi kwa mwaka 2016 wilayani Kilombero imebaini kuwapo tofauti ya takwimu za idadi ya wanafunzi na fedha zinazopelekwa kati ya shule na idara ya elimu.

Utafiti huo umefanyika kupitia mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma katika sekta ya elimu ambao umetekelezwa na shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na maendeleo Kilombero (KGCD) chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society ambao umefanyika kwa miezi sita kwa gharama ya Sh34 milioni.

Akiwasilisha ripoti ya ufuatiliaji huo, Mratibu wa KGCD, Christina Kulunge alisema takwimu katika shule 22 zinaonyesha Shule ya Nganyangila ilikuwa na idadi ya wanafunzi 527 wakati hali halisi ni kuwa ina wanafunzi 393, huku Shule ya Mkamba takwimu za wilaya zinaonyesha ilikuwa na wanafunzi 1,205 wakati idadi ni 1,034.

Alisema utafiti ulibaini tofauti ya fedha zinazoingia shuleni na taarifa zilizopo wilayani na idadi ya walimu kati ya shule na wilaya, ukosefu wa miundombinu, upungufu wa nyumba za walimu, madarasa, fedha za ruzuku zilizofika shule na za maendeleo.

Kulunge alisema changamoto nyingine ni ukosefu wa taarifa za mapato na matumizi za kila robo mwaka katika mbao za matangazo, ushiriki mdogo wa wananchi katika maendeleo ya shule, michango hafifu ya maendeleo ya shule kutoka kwa wazazi, uhaba wa madawati, walimu wa hisabati na sayansi na upungufu wa matundu ya vyoo.

Mratibu huyo alisema wananchi walitoa mapendekezo yakiwamo ya ujenzi wa vyoo vya walimu na wanafunzi, nyumba za walimu, kuongeza idadi ya walimu na fedha za ruzuku kwa wakati.

Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Peter Singo alikiri kuwapo upungufu huo na kwamba kamati za shule zimepewa mafunzo ya kufahamu wajibu wao tofauti na awali.
Habari kwa hisani ya Muungwana Blog
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment