Writen by
sadataley
11:21 AM
-
0
Comments
Na.Alex Matias,Dar es salaam
Nahodha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania
(Taifa Stars), Mbwana Samatta amedai mabadiliko ya kikosi cha timu hiyo
yaliyofanywa na Kocha Mkuu, Salum Mayanga hayawezi kuathiri nguvu na
mipango yao ya kupambana katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Botswana
utakaopigwa jioni ya Leo uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Alisema Kocha Mayanga aliamua kufanya
mabadiliko hayo kutokana na kutambua udhaifu uliopo kwenye kikosi hicho,
hivyo kuamua kuwaita wachezaji wengine wapya ambao wataleta chachu ya
ushindi kwa timu hiyo iliyo katika nafasi ya mbaya ya msimamo wa viwango
vya Shirikisho la Soka Duniani(FIFA) vilivyotolewa hivi karibuni.
Samatta alisema ni kweli timu ya Taifa
inahitaji wachezaji wazoefu watakaoendeleza mbinu zitakazotolewa na
Kocha Mkuu lakini wengi wa wachezaji wakongwe waliopo kwenye timu hiyo
walishindwa kuonesha uwezo wao na hatimaye kuipeleka timu mahali pasipo
stahili kuelekea.
“Nasikia jinsi watu wanavyolaumu uamuzi
uliofanywa na Kocha Mayanga, lakini mi nataka niwaambie ukweli
Watanzania kwamba hawa wachezaji ambao wanawasema ni wakongwe ni lazima
na wao wakae pembeni wawapishe wachezaji wapya waoneshe uwezo na kitu
kipya walichokuwa nacho ambacho kitakuja kuliinua taifa katika anga la
kimichezo,” alisema Samatta.
Kwa upande wake Kocha Mayanga, alisema
mchezo huo ni wa kwanza kwake utampatia nafasi ya kujua mapungufu na
uhiamara wa kikosi chake kabla ya kuelekea kwenye michuano ya AFCON
inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi Juni mwaka huu.
Alisema kutokana na mazoezi mazuri
waliyoyafanya kwa siku nne mfululizo yatawasaidia kuibuka na ushindi
mkubwa pamoja picha ya ubora wa kikosi hicho chenye malengo ya kupanda
maradufu kwenye viwango vya FIFA.
Alidai anaamini wachezaji walioitwa
kwenye kikosi hicho watatumia akili na nguvu zao zote ili kuhakikisha
Botswana haichomoki na ushindi wa aina yoyote ile huku akiwataka
watanzania kujenga imani na kikosi hicho chenye wachezaji vijana zaidi.
“Kwenye kikosi chetu hiki safari hii kuna
wachezaji wengi ambao ni vijana, niliwaamini na ndio maana nikaamua
kuwaita kwenye kikosi change, kwahiyo Watanzania tarajieni makubwa zaidi
katika mchezo wetu huu wa kesho(leo) utakaopigwajijini Dar es Salaam,”
alisema Mayanga.
Alisema ni vigumu kutoa ahadi katika
mchezo wa mpira wa miguu kutokana na kwamba hawajui timu wanayokwenda
kushindana nayo imejiandaa vipi dhidi ya mchezo huo ambao unaumuhimu
mkubwa kwa pande zote mbili.
Wakati huohuo, Kocha wa Timu ya Botswana,
Peter Buttler alisema wanauchukulia mchezo wao wa kirafiki na Taifa
Stars kuwa ni zaidi ya wa kirafiki kutokana na kuona umuhimu uliopo
kwenye mchezo huo ambao unatambuliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika
(CAF) na (FIFA).
“Tumekuja Tanzania kupambana na naomba
niwashukuru kwa ukarimu wao wote waliotuonesha ila kiukweli ni lazima
tuibuke na ushindi kwa gharama yoyote ile kwa sababu tunataka tupande
zaidi kwenye msimamo wa viwango vya soka katika mataifa ya Afrika
tofauti na hivi ilivyo sasa,” alisema Buttler.
Mbali na hilo, Msemaji wa Shirikisho la
Soka Tanzania(TFF), Alfred Lucas alitoa taarifa za kubadilishwa kwa
kiwango cha chini cha gharama za kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo
ambapo hapo awali ilikuwa ni Tsh. 5,000 na sasa kuwa ni Tsh.3,000.
No comments
Post a Comment