Writen by
sadataley
12:56 PM
-
0
Comments

Ndugu zangu,
Nelson Mandela kwenye safari yake ya
kwanza kwenda Ethiopia alifika kwanza Dar es Salaam, na ndiko alikosahau
viatu vyake. Kisha akaelekea Khartoum, Sudan.
Tunasoma, kuwa akiwa pale Sudan, baadae
akaelekea Ghana. Kule Ghana Mandela alikutana na Oliver Tambo, kiongozi
wa ANC aliyekuwa akiishi na kufanya kazi za ANC akiwa mafichoni. Nje ya
Afrika Kusini.
Mandela alikuwa hajaonana na Oliver
Tambo yapata miaka miwili. Alishangaa kumwona Oliver Tambo amebadilika,
si yule aliyekuwa akitokea katika staili ya mavazi ya kihafidhina.
Oliver Tambo akawa ni mtu aliyefuga madevu na staili ya mavazi
iliyobadilika. Alionekana mpiganaji zaidi.
Na hatimaye Mandela akafika Addis Ababa,
Ethiopia. Akiwa Ethiopia, na kwa kupitia maandiko kwenye kitabu chake ‘
Long Walk To Freedom’, Mandela anasimulia; kuwa ilikuwa ni mara yake ya
kwanza kukutana na Mfalme aliyeongoza dola yake katika Afrika. Ni
Mfalme Haile Selassie. Mandela alishangaa sana kumwona Mfalme mwembamba
kwa maumbile lakini mwenye kuonyesha kuwa ni mwenye mamlaka makubwa.
Siku ya pili yake tu, Mandela
aliuhudhuria gwaride la kijeshi ambapo Mfalme Haile Selassie alikuwa
mgeni rasmi. Mandela ikawa mara yake ya kwanza kuona gwaride la
wanajeshi mia tano Waafrika weusi likiongozwa na makamanda weusi. Jambo
hilo lilimfurahisha na kumtia nguvu Mandela.
Mandela anaielezea zaidi Ethiopia, nchi
ambayo zamani ikiitwa Abyssinia. Kuwa ni dola iliyokuwapo kabla ya
kuzaliwa Kristo. Inasemwa, kuwa Ethiopia ni himaya iliyoasisiwa na mwana
wa Mfalme Suleiman na Malkia wa Sheba.
Hata kama Ethiopia imepata kuvamiwa mara
zaidi ya 12, lakini, Ethiopia inabaki kuwa ni chimbuko la harakati za
kupigania utaifa kwa bara la Afrika. Ethiopia ndio dola ya Kiafrika
iliyoanza kupambana na ukoloni, na si mara moja. Mfalme Menelik
alipambana na kuwashinda wavamizi wa Kiitalia karne iliyopita.
Na mwaka 1930 Mfalme Haile Selassie
akatwaa mamlaka ya himaya ya Ethiopia. Mandela anakumbuka alikuwa na
umri wa miaka 17 tu, pale Fashist Mussolini wa Italia alipoivamia
Ethiopia. Ni uvamizi uliomfanya Mandela sio tu azidi kumchukia
Mussolini, bali kuuchukia ufashisti kwa ujumla wake.
Mfalme Haille Selassie akalazimika
kuikimbia Ethiopia kufuatia uvamizi ule wa mwaka 1936. Hata hivyo,
Mfalme Haile Selassie alirudi tena madarakani baada ya vikosi vya
washirika kuwaondoa Waitalia nje ya Ethiopia mwaka 1941.
Mandela anasema; kuwa Ethiopia siku zote
imekuwa na nafasi maalumu katika hisia zake. Kuitembelea Ethiopia ni
sawa na kuchimbua mizizi ya historia na kufahamu chimbuko la Uafrika
wake. Na kwa Mandela, anaamini, kuwa safari ya kwenda Ethiopia ilimvutia
zaidi kuliko ukichanganya safari za kwenda Ufaransa, Uingereza na
Marekani kwa pamoja. Na akawaza, kuwa kukutana na Mfalme Haile Selassie,
‘ Simba wa Yudah’ ingekuwa jambo kubwa sana. Ni sawa na kushikana
mikono na historia.
Kwa Mandela, Addis Ababa pamoja na kuwa
ni Makao Makuu ya Mfalme, haikuonekana kuwa ni mji mkubwa na wa kisasa.
Ilikuwa na mitaa michache, na hata mbuzi walionekana wakirandaranda
mitaani. Mandela anasimulia; kuwa Addis Ababa kulikuwa na mbuzi zaidi
kuliko magari barabarani. Ilikuwa ni tofauti kubwa na jiji la
Johannesburg.
Ethiopia haikuonekana pia kuwa mfano
katika demokrasia. Hakukuwa na vyama vya siasa wala mgawanyo wa
madaraka. Ni Mfalme tu aliyekuwa kila kitu.
Wakiwa Ethiopia, ikafika wakati wa
Mandela na Oliver Tambo kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Afrika,
ambapo, maombi ya ANC ya kutambuliwa rasmi yangejadiliwa pia.
Mandela na Tambo wakashangazwa kugundua,
kuwa maombi yao yameshakwamishwa. Ni mjumbe kutoka Uganda
aliyeyakwamisha akidai kuwa ANC ni chama cha kikabila.
Ni hapa, Mandela anakutana na changamoto
inayomlazimisha, mbele ya viongozi wa Kiafrika, ajenge hoja zenye
mashiko za kuifanya ANC iliyochafuliwa na PAC isafishike na ikubalike.
PAC walikipakazia kwa viongozi wa Kiafrika, kuwa Chama Cha ANC ni chama
cha kikabila. Ni hapa pia, Mandela kijana alipoanza kuonyesha uwezo na
karama alizo nazo katika uongozi.
Mandela akawa mtu wa pili kuongea baada
ya hotuba ya ufunguzi ya Mfalme Haile Selassie. Jinsi Mandela
alivyopambana kuitetea ANC, mbele ya ' Simba wa Yudah, Mfalme Haille
Selassie, ni simulizi nyingine.
Maggid Mjengwa.
No comments
Post a Comment