Monday, May 22, 2017

Rais mpya wa Ufaransa asisitiza askari wa nchi hiyo kubakia Mali

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema nchi yake itaendelea kubeba mzigo wa kuendesha mapambano ya kijeshi dhidi ya makundi ya wanamgambo wa kitakfiri wenye misimamo ya kufurutu ada kaskazini na magharibi mwa Afrika lakini ameitaka Ujerumani itoe msaada kufanikisha kampeni hiyo.
Macron aliyasema hayo jana Ijumaa nchini Mali, katika safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipochaguliwa kuwa rais mpya wa Ufaransa tarehe 7 ya mwezi huu wa Mei.
Hatua ya kiongozi huyo kuichagua Mali kwa safari yake ya kwanza kama Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ufaransa ni kutimiza ahadi aliyotoa ya kutembelea vikosi vya Ufaransa vinavyopambana na wanamgambo wa kitakfiri wenye misimamo ya kufurutu mpaka.
Akizungumza na mwenyeji wake Rais Ibrahim Boubacar Keita, Macron alisema Ufaransa inatimiza ahadi iliyotoa ya kuwa pamoja na serikali ya Bamako kuanzia awali katika vita hivyo na kwamba safari yake nchini humo ni ithbati ya kuendelea kutekeleza ahadi hiyo.
Aidha katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari katika mji wa Gao waliko askari wapatao 1,600 wa Ufaransa, Emmanuel Macron alisema kuna haja ya kuimarishwa hatua za kijeshi kwa sababu kuna ishara kwamba wanamgambo hao wameanza kujipanga upya.
Rais Ibrahim Boubacar Keita, Macron wa Mali (kulia) na mgeni wake Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa
Hata hivyo ametaka nchi nyengine wanachama wa Umoja wa Ulaya na hasa Ujerumani zichangie operesheni hizo za kijeshi kwa kutoa msukumo pamoja na vifaa vinavyohitajika.
Ufaransa imekumbwa na wimbi la mashambulio ya makundi ya kigaidi na kitakfiri ambayo yameua zaidi ya raia 230 wa nchi hiyo ndani ya ardhi Ufaransa yenyewe katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Mwaka 2013 Ufaransa iliingilia kijeshi nchini Mali ambalo ni koloni lake la zamani kwa kile kilichotajwa kuwatimua wanamgambo wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda waliokuwa wameliteka na kulikalia eneo la kaskazini mwa nchi hiyo mwaka mmoja kabla yake. Tangu wakati huo Ufaransa imeshatuma askari wapatao 4,000 katika eneo la Sahel kuwasaka wanamgambo hao katika eneo hilo kupitia kikosi cha pamoja na mataifa ya eneo hilo cha Barkhane.../ 
Parstoday.com
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment