Writen by
sadataley
1:51 PM
-
0
Comments
Marais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda wametiliana saini tamko la pamoja la kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza baada ya kutia saini tamko hilo, Rais Magufuli alimshukuru Rais Museveni kwa hatua ambayo Tanzania na Uganda zimefikia katika mradi wa bomba hilo la mafuta. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa, mradi huo ni matokeo ya urafiki na udugu wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili. Rais Magufuli aidha amesema, mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi za Uganda, Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika nzima.
Alitaja sababu za bomba hilo kupitia Tanzania kuwa ni uwepo wa amani, uzoefu wa Tanzania katika uendeshaji wa miradi ya mabomba ya mafuta na gesi, jiografia nzuri ya usafirishaji mafuta, ardhi na ubora wa bandari ya Tanga.
Kadhalika Rais Magufuli amesema kwamba, mradi huo utazinufaisha nchi za Afrika Mashariki yakiwemo mashirika ya ndege ambayo yatapata mafuta kwa gharama nafuu na hivyo kukua zaidi kibiashara.
Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Hoima–Tanga wenye urefu wa kilometa 1,443 zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania, utagharimu dola za Marekani bilioni 3.55. Hafla ya kutia saini tamko hilo ilifanyika jana Ikulu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, wanasheria wakuu wa serikali, wakurugenzi na viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusika katika mradi huo.
No comments
Post a Comment