Writen by
sadataley
7:38 AM
-
0
Comments
Polisi ya Uingereza imemtangaza Salman Abidi kuwa muhusika mkuu wa mripuko wa kigaidi katika mji wa Manchester nchini humo.
Kwa mujibu wa viongozi wa polisi, Salman Abidi mwenye umri wa miaka 22 alizaliwa Uingereza huku akiwa na asili ya Libya. Kijana huyo alilipua bomu lenye nguvu kubwa ndani ya ukumbi mmoja wa burudani mjini Manchester ambapo watu 22 walipoteza maisha na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa. Tukio hilo ni kubwa kuwahi kutokea nchini Uingereza tangu lilipojiri tukio la utegaji bomu katika njia ya reli mjini London hapo mwaka 2005 ambapo zaidi ya watu 50 walipoteza maisha katika tukio hilo. Hivi sasa Ulaya ikiwemo Uingereza inakabiliwa na wimbi jipya la ugaidi wa ndani. Hii ni kusema kuwa, miaka michache iliyopita, aghlabu ya mashambulizi ya kigaidi yaliyokuwa yakishuhudiwa barani Ulaya, yalikuwa yakitekelezwa na magaidi kutoka nje ya bara hilo.
Kwa mantiki hiyo walihesabiwa kuwa ni magaidi wa kigeni ambapo pia kulihamasishwa mapambano kwa ajili ya kuwamaliza maadui hao wa kigeni. Hata mifumo ya intelejensia na usalama wa mataifa ya Ulaya pia iliimarishwa kwa ajili ya kutambua, kufuatilia na kukabiliana na magaidi hao wa kigeni. Kwa mujibu wa viongozi wa usalama barani Ulaya, katika miaka ya hivi karibuni idara hizo za intelejensia zimefanikiwa pakubwa kusambaratisha mashambulizi kadhaa ya magaidi wa kigeni. Hata hivyo hii leo baadhi ya watu waliozaliwa katika jamii hizo hizo za Ulaya ndio wanaohusika na mashambulizi hayo ya kigaidi ambayo yanapelekea makumi ya raia wa mataifa hayo kuuawa. Salman Abedi ni mmoja ya watu hao ambaye alizaliwa, kulelewa na kusomea hukohuko nchini Uingereza. Hata hivyo kufuata fikra potofu, kufungamana na mafundisho yaliyo kinyume na dini ya Uislamu na pia athari mbaya inayotokana na mazingira ya kijamii na kiutamani barani Ulaya, huwasukuma vijana hao kufanya mauaji, ukatili na ugaidi. Pamoja na hayo kunajitokeza swali hili kwamba je, ni kitu gani kinachochangia kijana wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani au Marekani kumshambulia raia mwenzake?
Kuhusiana na hilo kunaibuka nukta moja isiyoweza kuepukika nayo ni hii kwamba, nchi za Magharibi ikiwemo Marekani zinakabiliwa na wimbi la ugaidi wa ndani. Aina hii ya ugaidi ni hatari zaidi kuliko ule ugaidi unaotoka nje. Kwa miaka mingi sasa vyombo vya intelejensia na usalama barani Ulaya na Marekani, vimeufahamu ugaidi kuwa wa eneo la magharibi mwa Asia pekee. Hatua kali za usalama wa kimipaka zilizochukuliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Schengen barani Ulaya, zinaweza kuandaa mazingira ya kuzuia kuingia magaidi wa kigeni ndani ya bara hilo. Hata hivyo kuwatambua mamia ya vijana walioathirika na fikra za ukatili na ugaidi katika maeneo tofauti ya kijamii, ni suala ngumu sana kwa vyombo vya upepelezi na usalama vya nchi hizo. Vijana wanaweza kwa urahisi kutengeneza mada za miripuko na aina nyingine za silaha bila kujulikana na vyombo husika vya usalama katikanchi hizo.
Kwa kuzingitia kuwa, vijana hao wamezaliwa ndani ya mataifa hayo ya Ulaya huku wakiwa wameishi kwa miaka mingi ndani ya jamii ya nchi hizo, wanaweza kuingia mahala popote kama vile kumbi, vituo vya usafiri na maeneo mengine ya kijamii na kutekeleza mauaji. Hii ni katika hali ambayo hivi sasa vyombo vya usafiri binafsi hususan magari ndiyo yanatumiwa na vijana wengi kwa ajili ya kutekeleza hujuma za kigaidi. Alaa kulli hal, tajriba ya kihistoria inaonyesha kwamba, kukabiliana na matukio ya uhalifu kama vile ugaidi, hususan ugaidi wa ndani hakuwezi kufikia natija tarajiwa kwa kutumia hatua kali za kiusalama na mashinikizo. Bila shaka kuondoa hatari hiyo kunahitajia kufanyika uchunguzi wa kina ili kuwatambua watu wenye misimamo ya kigaidi.
PARSTODAY
No comments
Post a Comment