Friday, June 2, 2017

Hatimaye Trump aiondoa Marekani kwenye makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi ya Ufaransa

Rais Donald Trump wa Marekani sambamba na kutangaza kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015, amesema kuwa makubaliano hayo hayana faida yoyote kwa Marekani.
Akitangaza kuiondoa Marekani katika makubaliano ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu ya carbon dioxide ambayo ni moja ya sababu za mabadiliko ya tabianchi duniani, Trump amesema: "Tunafanya juhudi za kuanzisha mazungumzo mapya kwa ajili ya kuandika mkataba ulio bora na ni lazima mazungumzo hayo yawape kipaumbele cha kwanza wafanyakazi wa vibarua wa Marekani." 
Kadhalika Rais Doland Trump ameongeza kuwa, mkataba wa Paris umewaletea raia wa Marekani ongezeko la gharama isiyoendana kiasi kwamba, kwa mkataba huo Marekani imepoteza nafasi nyingi za kazi hususan katika uga wa viwanda vya utengenezaji magari na vinginevyo. Baada ya kutangaza kuiondoa nchi yake katika mkataba wa Paris, Trump pia amesema: "Mimi nimechaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa Pittsburgh (mji mkubwa wa pili wa jimbo la Pennsylvania) na sio kwa ajili ya Paris." Mwisho wa kunukuu. Hayo yanajiri katika hali ambayo katika siku za hivi karibuni, viongozi mbalimbali wa nchi za Magharibi akiwemo Kansela wa Ujerumani Bi, Angela Merkel na mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, sambamba na kukosoa vikali uamuzi wa Trump wa kutaka kuiondoa Marekani katika mkataba wa Paris wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, waliitaka Washington kufungamana na mkataba huo.
Weledi wa mambo wanaamini kwamba, hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mkataba huo itaisababishia sayari ya dunia ongezeko kubwa la joto kali, hasa kwa kuzingatia kuwa, Marekani ndio chanzo kikuu cha kuongezeka joto hilo dunia. Awali katika katika kikao cha viongozi wa kundi la G7 Trump alitangaza kuwa, Washington inahitaji muda zaidi wa kufikiria juu ya kuendelea kuunga mkono makubaliano ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa mtazamo wa rais huyo wa Marekani, kimsingi suala la ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi ni mambo yasiyo na ukweli wowote na kwamba eti mambo hayo yamebuniwa tu na Wachina.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment