Friday, July 14, 2017

Tanzania yatakiwa kuongeza juhudi za kukabiliana na ongezeko la ndoa na mimba za utotoni

Serikali ya Tanzania imetakiwa kuongeza juhudi katika kukabiliana na wimbi la ongezeko la ndoa na mimba za utotoni linalokatisha ndoto za kielimu za wasichana katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wito huo umetolewa  na mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu barani Afrika  Graca Machel wakati wa ziara maalumu ya kukagua miradi ya afya mkoani Dodoma.  Graca Machel ambaye ni mjane wa mke wa rais  wa zamani wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela amesema kuwa, inasikitisha sana kuona namna ambavyo maisha ya wasichana wadogo yanakatishwa na baadhi ya watu wazima wasiokuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu.
Amesema kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi barani afrika ambazo zinakabiliana na changamoto kubwa ya ndoa za utotoni ambazo kwa kiasi kikubwa zinawanyima wasichana haki zao za msingi za kikatiba na kibinadamu.
Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu amewataka viongozi wa serikali ya Tanzania katika ngazi zote kushirikiana kwa karibu na viongozi wa mila na dini ili kupiga vita vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya wasichana wadogo katika nchi hiyo.
Amesema, wasichana wana haki ya kupata elimu, angalau ya kidato cha nne halafu ndiyo wawe katika nafasi nzuri ya upevu wa akili wa kuchagua hatma zao za ndoa na maisha mengine na kuonya kuwa, jitihada za seikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli ya kutoa elimu bure haitazaa matunda tarajiwa kama janga hilo halitakomeshwa.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment