Writen by
sadataley
11:17 AM
-
0
Comments
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania
Kundi la Mashirika ya Kimataifa 18 yanayotetea haki za binadamu limeitaka Tanzania kuacha kuzinyanyasa asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu hasa zile zinazotetea haki ya wanafunzi waliopata ujauzito kurudi shuleni.
Taarifa ya kundi hilo la mashirika yanayotetea haki za binadamu ya kimataifa limeitaka serikali ya Tanzania kuyaacha mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya shughuli zake bila ya wasiwasi wa kuchukuliwa hatua.
Hivi karibuni Mwigulu Nchemba , Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alinukuliwa akionya kwamba wizara yake haitasita kulifutia usajili shirika lolote lile lisilo la kiserikali linalotetea mapenzi ya jinsia moja na wanafunzi kurudi shuleni baada ya kuwa wajawazito.
Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo, iliyotiwa saini na mashirika makubwa ya kimataifa kama vile Human Rights Watch na Amnesty International pia imeunga mkono msimamo wa kundi la asasi za kiraia lenye wanachama 25 ambalo wiki iliyopita kwa pamoja lilitoa tamko lake kutaka serikali iwaruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kurudi shuleni baada ya kuwa wamejifungua.
Kundi hili la mashirika ya asasi za kiraia za kimataifa limeitaka serikali ya Rais John Pombe Magufuli kuelekeza nguvu zake zaidi katika kuwapatia wananchi wake huduma bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile.
Rais Magufuli na viongozi wengine wa ngazi ya juu ndani ya serikali yake wameendelea kutilia mkazo msimamo wao kwamba serikali hiyo haitaruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kurudi shuleni baada ya kuwa wamejifungua.
Parstoday
No comments
Post a Comment