Saturday, August 12, 2017

Bill Gates awa gumzo kila kona

UJIO wa tajiri namba mbili duniani, Bill Gates umezua gumzo maeneo mbalimbali ya wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga huku baadhi ya watu wakishindwa kuamini kuwa ni kweli tajiri huyo alifika juzi hapa.

Baadhi ya wakazi wa wilaya hii wamesema ni jambo la ajabu kwa bilionea huyo kuja nchini na kutembelea wilaya ya Tanga badala ya maeneo mengi ya kifahari ambayo angeweza kwenda kwa hadhi aliyonayo.

Hata hivyo, Gates ambaye jana alikuwa na mazungumzo na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam, alifika wilayani Muheza kukagua nyumba tano ambazo zitakuwa maalum kwa ajili ya utoaji dawa za kinga ya matende na mabusha ambazo zitaletwa naye.

Mazungumzo kati ya tajiri huyo na Rais Magufuli yalihudhuriwa na uongozi wa wizara yenye dhamana ya Afya.

Akizungumza na Nipashe kuhusu ujio wa mtu huyo mashuhuri hapa Muheza, Juma Selemani alisema wengi kati ya watu aliozungumza nao walionyesha kushangaa kusoma kuwa Gates alifika katika kijiji cha Kicheba bila wakazi wa Muheza kufahamu ujio wake.

Alisema kutokana na ukimya wa ziara hiyo imekuwa vigumu kwa watu wengi kauamini tukio hilo.

Kwa upande wake, John Saimon, mkazi wa kijiji cha Mkuzi alisema aliamini kweli tajiri huyo amefika Muheza baada ya kuona picha akiwa na viongozi wa wilaya.

Lakini akalalamikia wakazi kutopewa taarifa ili wampokee mgeni huyo kwa kuwa alileta neema katika wilaya ya Muheza.

Gates (61), ni raia wa Marekani ambaye alipoteza nafasi ya kwanza miongoni mwa mabilionea wa dunia mwezi uliopita.

Alishika nafasi ya pili, kwa mujibu wa Jarida la Forbes, baada ya kupitwa na Jeff Bezos, mwanzilishi na mmilikiwa mtandao wa manunuzi wa Amazon.co ambaye anakuwa mtu wa kwanza kuvuka utajiri unaofikia dola za Marekani bilioni 90 (Sh. trilioni 210).

Gates mwenye utajiri wa dola za Marekani bilioni 89.9 (Sh. trilioni 199) na ambaye alikuwa Muheza kutembelea miradi ya kijamii, ni mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya utengeneza mifumo ya kompyuta ya Microsoft.

Akiwa Kicheba, tajiri huyo alikula chakula na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kicheba.

Akizungumza na mwandishi wa Nipashe, diwani wa kata ya Kicheba, Hamisi Mkodingo alisema kuwa Gates aliwasili katika kata yake akiwa ameongozana na viongozi hao wa wilaya ya Muheza.

Mkodingo alisema kuwa baada ya tajiri huyo kufika Kicheba, alisomewa taarifa ya wilaya hiyo na baadaye alitembelea nyumba tano ambazo zitakuwa maalum kwa ajili ya utoaji dawa za kinga ya matende na mabusha.

Juni 2006, Gates alitangaza kuwa ataachia polepole majukumu yake kama mtendaji mkuu wa Microsoft na kujikita katika shirika
lake na mkewe la hisani la Mfuko wa Bill&Melinda Gates (BMGF), kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa Wikipedia.

BMGF ilianzishwa mwaka 2000 na kwa mujibu wa Wikipedia, inasemekana kuwa mfuko mkubwa zaidi duniani unaoendeshwa kwa uwazi.

Lengo kuu la mfuko huo wenye makao yake katika jiji la Seattle, jimbo la Washington, ni, kidunia, kuboresha utoaji huduma za afya na kupunguza umasikini is controlled by its three trustees: Bill and Melinda Gates, and Warren Buffett.

Diwani Mkodingo alisema uongozi wa kata ya Kicheba na wilaya ziliandika barua ya kumuomba tajiri huyo ujenzi wa kituo cha afya cha kata na ujenzi wa maabara ya sekondari ya kata ya Kicheba ambao haujakamilika.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Mlelwa alisema kuwa ni fursa kubwa kutembelewa na tajiri huyo duniani na kwamba anaamini wilaya ya Muheza itasaidiwa mambo mbalimbali ya maendeleo.

BILL GATES NI NANI?
Bill Gates ni raia wa Marekani ambaye aligundua program ya PC Software inayotumika kwenye kompyuta duniani, akiwa amewekeza kwenye teknolojia hiyo tangu mwaka 1975, kwa mujibu wa Wikipedia.

Amechangia kiasi kikubwa cha fedha kwenye taasisi za kijamii na tafiti za kisayansi kupitia taasisi ya BMGF na pia ana watoto watatu.

Hii mara ya sita kwa Bill Gates kutembelea Tanzania.

Mwaka 2011 alitembelea Tanzania akiwa na mkewe na walikwenda Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya kuendeleza jitihada za kupambana na malaria.

Pia walikutana na watafiti na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (Ifakara Health Institute), na kuona shughuli za kukinga malaria kupitia nyandarua vyenye dawa, pia walitembelea vijiji vya Mapinga na kuzungumza na wananchi.

Mara zote alizotembelea nchini kipindi cha Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alikutana naye na kufanya mazungumzo na alimshukuru kwa jitihada za kusaidia wananchi wa kawaida.

Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete, matarajio ni kuwa Gates pia atatembelea Hifadhi ya Serengeti na kwamba itakuwa ni mara ya tano.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment