Writen by
sadataley
1:02 PM
-
0
Comments
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewapongeza Wakenya kwa kushiriki kwa amani katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8.
Guterres amesema viongozi wanaolalamikia matokeo ya uchaguzi wawasilishe malalamiko yao kwenye taasisi zenye mamlaka kikatiba ya kushughulikia mizozo ya uchaguzi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitizia umuhimu wa mazungumzo ili kuondoa mivutano na hali ya wasiwasi nchini Kenya.
Guterres aidha ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kufikisha ujumbe wa wazi kwa wafuasi wao wa kuwasisitiza wajiepushe na machafuko na vitendo vya utumiaji nguvu.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa UN, umoja huo kwa mashauriano ya karibu na Umoja wa Afrika (AU) pamoja na washirika wengine wa kieneo na kimataifa utashirikiana kikamilifu na uongozi wa kisiasa wa Kenya pamoja na wadau wengine husika ili kukamilisha kwa mafanikio mchakato wa uchaguzi wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya IEBC, Rais Uhuru Kenyatta aliyegombea urais kwa tiketi ya chama cha Jubilee aliibuka mshindi baada ya kujizolea kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura zote huku mshindani wake mkuu Raila Odinga wa muungano wa upinzani wa NASA akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 ya kura zote.
Hata hivyo muungano wa upinzani wa NASA umeyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais na kusisitiza kuwa zoezi hilo lilikumbwa na wizi wa kura. NASA aidha imesisitiza kuwa haitakwenda mahakamani kupinga matokeo hayo.
Kwa mujibu wa ripoti rasmi, hadi sasa watu 11 wameuawa kwa kupigwa risasi nchini Kenya katika mandamano na vurugu za kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Hata hivyo bila ya kutoa ushahidi wowote mrengo wa upinzani umedai kuwa jeshi la polisi limeua watu mia moja tangu yalipoanza maandamano ya kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumanne iliyopita.
Parstoday
No comments
Post a Comment