Wednesday, August 23, 2017

Maandamano ya Waislamu wa Uhispania ya kupinga ugaidi

Waislamu wa mji wa Barcelona nchini Uhispania wameandamana kwa mara ya pili katika kipinchi cha chini ya wiki moja wakilaani shambulio la kigaidi la Alkhamisi iliyopita huko Las Ramblas.
Waislamu hao walisikika wakipiga nara za kulaani ugaidi katika maandamano hayo. Baadhi ya nara zilizosikika katika maandamano hayo ni kama "Tusiwalaumu Waislamu", Uislamu hauungi mkono ugaidi", na sisi wote ni watu wa Barcelona.
Ikumbukwe kuwa, watu 13 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika shambulio la kwanza katika eneo la Las Ramblas katika mji wa Barcelona. Masaa machache baadaye mwanamke mmoja aliaga dunia huko Cambrils wakati gari lilipoingia katika eneo la waendao kwa miguu na kisha kuwagonga.
Siku nne ya baada ya tukio hilo, polisi ya Uhispania imetangaza kuwa, imemuua Younes Abouyaaqoub aliyetekeza shambulio la kigaidi la Alkhamisi wiki iliyopita katika mji wa Barcelona. Vyombo vya habari vya Uhispania vimetangaza kuwa, mshukiwa huyo alipigwa risasi eneo la Subirats, karibu na Sant SadurnĂ­ d'Anoia lililoko umbali wa kilomita 60 kutoka Barcelona na alionekana akiwa amevaa mkanda wa kujilipua.
Eneo la Las Ramblas palipotokea shambulio la kigaidi
Kama ilivyokuwa kwa matukio mengine ya kigaidi yaliyotokea katika miaka ya nyuma barani Ulaya, mara hii pia Waislamu walituhumiwa kuwa, ndio wanaoeneza fikra za kufurut ada na ugaidi barani humo. Baada ya shambulio la kigaidi la Barcelona, kuliripotiwa habari za kushambuliwa misikiti na vituo kadhaa vya Kiislamu nchini Uhispania.
Siku ya Jumamosi tareher 19 Agosti msikiti mmoja katika mji wa Seville ulishambuliwa na makundi ya wabaguzi. Watu hao wenye chuki na Uislamu walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na kuandika maneno ya kibaguzi katika kuta za msikiti huo. Maneno hayo ya kibaguzi yalikuwa dhidi ya Waislamu na raia wa kigeni kutoka nchi za kaskazini mwa Afrika. Aidha moja ya maneno hayo yaliyoandikwa katika kuta za msikiti huo yalikuwa yakiwatishia Waislamu kwamba, watauawa kwa kukatwa vichwa.
Younes Abouyaaqoub aliyetekeza shambulio la kigaidi la Alkhamisi wiki iliyopita katika mji wa Barcelona
Aidha matukio kama hayo yalishuhudiwa pia katika mji wa Granada ambapo kundi la wabaguzi liliuchoma moto msikiti mmoja mjini humo na kuwafanya wanawake na watoto waliokuwa ndani ya msikiti huo kukimbia ili kuokoa maisha yao. Wabaguzi hao walishambulia msikiti huo wakiwa na bango la maandishi yasemayo: Kila mwenye kuusaidia kifedha msikiti huu anaunga mkono ugaidi."
Mtandao wa Habari wa NBC News uliandika kuwa, akthari ya wachambuzi wa mambo wana wasiwasi na suala la kuzidi kuwa magumu maisha ya Waislamu wengi wanaoishi katika mji wa Granada.
Mwandishi mmoja wa habari ambaye ni mkazi wa Barcelona sambamba na kuonyesha wasiwasi wake kuhusiana na athari mbaya za mashambulio ya kigaidi ya Daesh nchini Uhispania kwa maisha ya Waislamu wa nchi hiyo amesisitiza kwamba, haipaswi kuwatambua watu wote wa Catalonia na Waislamu kwamba, ni watenda jinai, kwa sababu tu mtu mmoja  wa eneo hilo ametenda jinai.
Msikiti wa Seville ulipochomwa moto
Katika ripoti yake, Shirika la Habari la Ufaransa  limeelezea wasiwasi uliozuka miongoni mwa Waislamju kutokana na anga ya chuki dhidi ya Waislamu iliyotanda katika mji wa Barcelona.
Licha ya tuhuma zote dhidi ya Uislamu, lakini madola ya Magharibi, asasi za kijasusi na kiusalama za Magharibi zinafahamu vyema kwamba, mafundisho ya Uislamu hayana uhusiano wowote na fikra za kufurutu ada za magaidi wa kitakfiri wa Daesh. Maandamano ya amani ya Waislamu mjini Barcelona ya kuungana pamoja na wahanga wa shambulio la kigaidi la wiki iliyopita ni ya kusisitiza kwamba, mafundisho ya amani ya Uislamu katu hayana uhusiano wowote ule na fikra za kigaidi za kundi la Daesh.
Parstoday 

« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment