Tuesday, September 19, 2017

Hatma ya kufanyika uchaguzi wa rais Kenya katika tarehe iliyopangwa bado haijajulikana hadi sasa

Duru za habari za Magharibi zimeripoti kuwepo suitafahamu kuhusiana na tarehe ya kufanyika uchaguzi wa rais wa marudio nchini Kenya.
Kampeni za uchaguzi nchini Kenya
Kinara wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Shirika la Habari la Ufaransa limeripoti kwamba, hali ya suitafahamu imeendelea kutanda juu ya tarehe rasmi ya kufanyika uchaguzi huo tangu kulipobatilishwa matokeo ya uchaguzi wa tarehe nane Agosti mwaka huu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, majaji wa Mahkama ya Kilele nchini Kenya wana muhula hadi tarehe 22 mwezi huu kutoa maamuzi kuhusiana na kufanyika kwa uchaguzi huo.
Kabla ya hapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC ilikuwa imetangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi huo wa marudio kuwa ni Oktoba 17, lakini hadi sasa hakuna maandalizi yaliyofanywa kwa ajili ya uchaguzi huo. Baadhi ya duru za kisiasa zimeonyesha wasi wasi kwamba kuna uwezekano mkubwa uchaguzi wa marudio usifanyike katika tarehe hiyo. Wapinzani nchini Kenya wanapinga kufanyika uchaguzi huo ndani ya mwezi huo huku weledi wengine wakiamini kuwa uchaguzi utafanyika mapema ndani ya tarehe hiyo. Katika mazingira hayo, wapinzani wametishia kwamba ikiwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC itaendelea kupuuza matakwa yao, basi watasusia uchaguzi huo.
Kujiuzulu viongozi wa IEBC na kubadilishwa viongozi wanaohusika na maandalizi ya uchaguzi, ni miongoni mwa matakwa ya viongozi wa upinzani nchini humo. Siku chache zilizopita, kinara wa upinzani nchini humo, Raila Odinga alinukuliwa akisema kuwa, muungano wa upinzani wa NASA hautashiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 17 iwapo masharti waliyoyatoa hayatatekelezwa.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment