Writen by
sadataley
11:00 AM
-
0
Comments
Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga amemtuhumu Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Joseph Boinett kwa kupuuzia usalama wa majaji na kwamba anahatarisha maisha yao.
Wafuasi wa Jubilee wakiandamamana kupinga uamuzi wa Mahakama ya Juu wa kubatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta
Pamoja na kutoa tuhuma hizo katika tamko la Tume ya Majaji, Maraga amesema hilo halitawarudisha nyuma katika kuilinda katiba na pia wapo tayari kulipia kwa gharama yoyote.
Mtandao wa Gazeti la Daily Nation unamnukuu Maraga akisema: Tupo tayari kulipa gharama yoyote kutetea katiba na utawala wa sheria.
Tamko hilo linamlaumu Boinett kwa kupuuzia wito wa majaji wa kutaka wapewe ulinzi jambo ambalo linawaweka wao na mali zao katika hatari.
Taarifa hiyo imesema, kama viongozi wamechoka kuwa na mahakama imara, waitishe kura ya maoni iondolewe. Lakini kabla hilo halijafanyika, mahakama itaendelea kufanya kazi yake kama inavyostahili kwa kuzingatia katiba.
Wakati huo huo, jana polisi nchini Kenya walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta ambao walikuwa wakiandamana nje ya Mahakama ya Kilele mjini Nairobi wakipinga uamuzi wa mahakama hiyo kubatilisha uchaguzi wa Rais wa Agosti 8.
Waandamanaji hao waliwatuhumu majaji wa mahakama hiyo kuwa walitoa uamuzi ulio kinyume cha sheria wakidai kwamba, ingepaswa kuamuru kura zihesabiwe upya badala ya kurudia uchaguzi kufuatia kesi iliyowalishwa na mgombea urais aliyeshindwa, Raila Odinga wa muungano wa NASA akipinga kutangazwa Uhuru Kenyatta kuwa mshindi katika uchaguzi huo.
Parstoday
No comments
Post a Comment