Friday, September 22, 2017

Serikali yaufungia mgodi

Mkuranga. Serikali imeufungia kwa muda usiojulikana mgodi wa mchanga wa Kulagwa wilayani Mkuranga kutokana na shughuli zake kusababisha uharibifu wa mazingira na hasa kwa wakazi wa Kata ya Tengerea.

Miongoni wa uharibifu huo ni mmomonyoko wa ardhi unaosababishwa na wachimbaji wa mchanga.

Serikali pia imesema itaunda timu ya wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc); Wizara ya  Nishati na Madini;  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi;  Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Halmashauri ya Mkuranga kwa ajili ya kufanya utafiti na tathmini ya athari za mazingira zilizojitokeza. Kazi hiyo itafanyika kwa wiki mbili.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina amesema hayo leo Alhamisi akiwa ziarani eneo hilo.

Mpina amesema mbali ya uharibifu wa mazingira, hakuna ushirikishwaji wa kutosha kati ya wananchi na watu walionunua eneo hilo kwa ajili ya uchimbaji wa mchanga.

Amesema uchimbaji holela wa mchanga  umesababisha maisha kwa wakazi wanaozunguka eneo hilo kuwa hatarini na hasa wakati wa mvua.

Naibu waziri amesema timu hiyo itafanya kazi kwa wiki mbili na matokeo ya utafiti huo yatapelekwa ofisini kwake kwa hatua zaidi.

Mpina amesema baada ya timu kumaliza kazi, wahusika watakaobainika kusababisha uharibifu watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kulipa faini na kuyarejesha mazingira katika hali ya awali.

Diwani wa Kata ya Tengerea, Shaaban Manda amesema uchimbaji mchanga ni kero na unasababisha watu kushindwa kupata huduma ya kutosha ya maji kutoka katika mabwawa yaliyopo eneo hilo.

Amesema wachimbaji mchanga walipewa eneo dogo lakini sasa wanafika hadi katika makazi ya watu.

Mwananchi:
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment