Wednesday, December 13, 2017

Aliyeshinda kura ya maoni CCM ashikiliwa na TAKUKURU


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Singida inamshikilia mshindi wa kwanza kura za maoni CCM jimbo la Singida Kaskazini, Haider Ghulamali (46) kwa tuhuma ya kutoa rushwa ya Sh 2 milioni kwa ofisa usalama wa taifa.

Ghulamali ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha magodoro  mjini Dodoma inadaiwa alitoa rushwa hiyo ili ofisa usalama huyo amtolee taarifa nzuri kwenye vikao vya ngazi za juu aweze kuthibitishwa kuwa mgombea ubunge jimbo la Singida Kaskazini.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Joshua Msuya amesema Ghulamali amekamatwa jana Jumanne saa 8.30 mchana, maeneo ya Rafiki resort wakati akikabidhi rushwa hiyo iliyokuwa imehifadhiwa kwenye bahasha.

Msuya amesema Desema 11 mwaka huu, ofisi yake ilipata taarifa ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwa mmoja wa wana CCM anayewania ubunge jimbo la Singida Kaskazini ambaye ni Ghulamali.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo uchunguzi ulianza ikiwa ni pamoja na kuchunguza vitendo rushwa alivyofanya mtuhumiwa huyo, kabla na baada ya kura za maoni kupigwa.Kura hizo zilimpitisha Ghulamali aliyepata kura 606 kati ya kura 1009 zilizopigwa,” amesema.

Mkuu huyo amesema baada ya zoezi hilo kupita la kura za maoni mtuhumiwa kwa juhudi zake aliweza kupata namba za simu za ofisa wa usalama wa taifa ambaye walikuwa hawafahamiani.

“Baada kupata namba ya simu ya ofisa usalama taifa, Ghulamali aliweza kumpigia na akatoa maombi yake ya kusafishiwa taarifa kwenye vikao vya juu. Baada ya maombi hayo aliweza  kutoa rushwa ya shilingi milioni mbili na kumkabidhi ofisa huyo. Ndipo alipokamatwa na Takukuru waliokuwa wameweka mtengo,” alisema Msuya.

Alisema uchunguzi zaidi bado unaendelea kuhusiana na mtuhumiwa Ghulamali kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi wa kura za maoni.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment