Wednesday, December 13, 2017

Viongozi wa zamani Nicol wafikishwa mahakamani


Dar es Salaam. Kampuni ya Uwekezaji ya Nicol imefungua kesi ya madai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya aliyekuwa mwenyekiti wa bodi, Felix Mosha na aliyekuwa mtendaji mkuu, Kathleen Armstrong.

Kesi hiyo ya madai namba 282/2017 inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respius Mwijage.

Akina Mosha wametakiwa kupeleka utetezi Desemba 20,2017 na kesi imepangwa kutajwa Januari 24,2018.

Kampuni ya Nicol inaiomba Mahakama iamuru akina Mosha walipe Sh180.1 milioni ambazo ni gharama za hasara iliyoingia.

Pia, inaomba Mahakama iamuru wadaiwa warejeshe magari, walipe riba ya asilimia 26 na gharama za kesi.

Katika kesi hiyo, akina Mosha wanatetewa na wakili Herbert Nyange; huku kampuni ya Nicol ikiwakilishwa na wakili Benjamin Mwakagamba.

Inadaiwa katika hati ya madai kuwa Mosha licha ya kuondolewa uenyekiti na wanahisa  mwaka 2012 ameshindwa kukabidhi gari la ofisi aina ya Toyota Land Cruiser hivyo kusababisha ofisi ya Nicol kutafuta usafiri mwingine.

Kuhusu Armstrong anadaiwa akiwa amesimamishwa kazi baada ya kuondolewa na wanahisa, alishiriki  kutapanya mali za Nicol ikiwamo kuuza gari aina ya Mitsubishi bila idhini ya bodi au wanahisa.

Mahakama imeagiza Armstrong ambaye ni raia wa Marekani apelekewe notisi kwa njia sahihi.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment