Tuesday, February 13, 2018

Abbas na Putin wazungumzia nafasi ya US katika mgogoro wa Palestina

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas amemwambia Rais Vladimir Putin wa Russia kwamba nchi yake haitaikubali tena Marekani kuwa mpatanishi katika mgogoro wake na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika mkutano uliofanyika jana mjini Moscow, Abbas amesema Palestina inataka kupanua timu ya wapatanishi wa mgogoro huo, kwa kuzijumuisha pande nne za Russia, Marekani, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa Russia na Palestina mjini Moscow
Amesisitiza kuwa serikali ya Marekani ilipoteza nafasi yake ya kuwa mpatanishi wa pekee katika mchakato wa kutatua mgogoro kati ya Palestina na Israel kwa kukiuka sheria na maazimio ya kimataifa kutokana na hatua yake ya kichokozi ya kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa Israel. 
Jamii ya kimataifa zikiwemo nchi nyingi waitifaki wa Marekani imelaani hatua iliyochukuliwa tarehe 6 mwezi wa Disemba na Rais Donald Trump wa Marekani ambaye, kinyume na maazimio ya kimataifa, aliitangaza Quds Tukufu (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.  
Aidha alitangaza kuwa Marekani imeanzisha mchakato wa kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel Aviv, jambo ambalo lilizusha makelele na malalamiko kutoka kila kina dunia.

Parstoday.com
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment