Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na waliokuwa maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Mori Sinare na Sioi Solomon wanasota rumande kutokana na upande wa mashtaka kuendelea kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Wakili wa Serikali mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amesema leo Februari 16, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Kishenyi amedai kuwa upelelezi upo katika hatua za kukamilishwa na akaomba wapangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya kueleza hayo. Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa ameomba wapangiwe siku saba ili waweze kujua upelelezi umefikia katika hatua ipi.
Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hadi Machi 2, 2018 na kuutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi ili kila mshtakiwa ajue hatma ya maisha yake.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani 550 milioni kwa serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.
Wanadaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani 6 milioni, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani 6 milioni katika akaunti tofauti tofauti za benki.
Kati ya Machi 2013 na Septemba 2015, wanadaiwa kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi.
Mwananchi.
No comments
Post a Comment