Writen by
sadataley
9:09 PM
-
0
Comments
Ujumbe wa Papa Leo XIV kwa Siku ya 41 ya Vijana Ulimwenguni: Sherehe ya Kristo Mfalme 2026
Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Vijana Ulimwenguni, ngazi ya Kijimbo sanjari na Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu tarehe 22 Novemba 2026 yananogeshwa na kauli mbiu: "Jipeni Moyo! Mimi nimeushinda Ulimwengu: Ujasiri; Ushindi dhidi ya Ulimwengu; Ushindi wa upendo wa kujisadaka; Ujasiri wa unyenyekevu; Kristo Mfufuka anawakirimia waja wake amani, changamoto ni kufungua mioyo yao kwa Kristo Mfufuka! Tukutane Jimbo kuu la Seoul, Agosti 2027.
Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar es Salaam
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Vijana Ulimwenguni ngazi ya Kijimbo tarehe 22 Novemba 2026: “Jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu.” (Yn 16:33) Vijana wapendwa, Ninapenda kuwafikia ninyi nyote kupitia ujumbe huu na, zaidi ya yote, kumshukuru Mungu kwa zawadi mliyo nayo kwa Kanisa na kwa jamii. Yeye anawajua, anawapenda, na anawasindikiza katika safari yenu ya maisha. Roho wake anatia ndani yenu nyote licha ya tofauti zenu na kusambaa kwenu kote duniani hamu ileile ya mambo makuu na ya kudumu, naye anawasukuma kutafuta uhuru na ukweli. Kutoka kwa Mungu inatoka hamu yenu ya kupenda na kupendwa, pamoja na tumaini ambalo Roho Mtakatifu anahuisha mioyoni mwenu tumaini ambalo linaweza pia kuwa mwanga kwa wengine. Kwa haya yote, namshukuru Bwana. Tunajiandaa kuadhimisha Siku ya 41 ya Vijana Duniani katika Makanisa yetu mahalia mnamo tarehe 22 Novemba 2026 katika Sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mfalme wa Ulimwengu, huku tukitazamia pia Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni yatakayofanyika Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini mnamo Agosti 2027. Katika maandalizi ya matukio haya, ningependa kuwaachia maneno haya ya Yesu: “Jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu” (Yn 16:33). Maneno haya yatakuwa ndiyo kaulimbiu yetu katika miezi ijayo, na ninawaalika sasa kuanza kutafakari juu yake pamoja nami.
Ujasiri hutoka wapi?: Maneno ya Kristo yanaanza na mwaliko wa kuwa na ujasiri. Najua vyema kwamba, wakati mwingine, badala ya ujasiri, ni kutokuwa na uhakika au hofu ndiyo inayoweza kutawala ndani yetu, kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa kwanza. Wengi wenu mna maswali na mahangaiko yanayoelemea mioyo yenu. Labda mna wasiwasi kuhusu wakati ujao, mnahisi shinikizo la kufanikiwa na kuonekana wakamilifu, au mnapitia msongo wa kulinganisha maisha yenu na ya wengine, au na viwango vya kufikirika ambavyo havifikiki. Kutokana na ushawishi wa picha zilizopangwa kwa uangalifu kwenye mitandao ya kijamii, huenda mkaona ni vigumu kutambua na kukubali utambulisho wenu halisi. Hakika, mna kiu ya upendo wa dhati, kwani teknolojia haiwezi kuchukua nafasi ya ukaribu halisi wa kibinadamu; inaweza tu kuiga hisia za kujali na kuelewana. Baadhi yenu mnajua maana ya kupitia upweke, kukatishwa tamaa, au hofu ya kutotosheleza. Kwa sababu hizi, labda nanyi pia mmewahi kuhisi kama wanafunzi wa Yesu, wakivuka ziwa usiku kwa kutumia mashua ndogo. Upepo unazidi kuvuma kwa nguvu, mawimbi yanainuka, na ukingo wa ziwa unapotea gizani. Katika hali kama hizi ndipo tunaposikia mwaliko wa Injili wa kuwa na ujasiri. Yesu anawajia wanafunzi wake na kuwaambia: “Ni mimi; msiogope” (Yn 6:20). Hili ndilo hakikisho ninalotaka kuweka mioyoni mwenu: hata kabla hamjaanza kumtafuta Kristo, yeye tayari anawatafuta ninyi, akitembea juu ya maji yenye dhoruba ya maisha. Ujasiri wa Kikristo hautokani hasa na nguvu zetu wenyewe; unatokana na uwepo wake. Kristo mwenyewe hakupitia maisha yasiyo na dhoruba, wala hatuahidi maisha ya namna hiyo. Hata hivyo, hakuna giza wala mateso yaliyo na nguvu kuliko upendo wake. Hatakuacha kamwe. Anakualika katika urafiki naye na kukuomba umkabidhi safari yako binafsi pamoja na safari ya jumuiya zako. Hivyo basi, kubalini kukutana na Yesu Kristo ambaye anawatafuta, na mkabidhi kwake njia mnayopita, mkiwa watu binafsi na pia mkiwa pamoja. Kwa njia hii, mtahisi ujasiri mpya na wa kudumu ukikua ndani ya mioyo yenu.
Ushindi dhidi ya ulimwengu: Bwana Yesu, aliyewaendea wanafunzi wake akitembea juu ya maji, sasa anatuambia: “Jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu” (Yn 16:33). Pokeeni maneno haya kama ahadi inayoelekezwa binafsi kwa kila mmoja wenu, na kwa kaka na dada ambao mnashiriki nao safari yenu. Zaidi ya kuwa himizo tu, maneno haya ni zawadi. Kristo hasemi, “Ninyi mtaushinda ulimwengu.” Anasema, “Mimi nimeushinda ulimwengu.” Tunajua kwamba, katika kifungu hiki cha Injili, neno “ulimwengu” halimaanishi uumbaji wote uliofanywa na kupendwa na Mungu na uliokusudiwa kupata wokovu, bali linamaanisha “ulimwengu wa giza” (taz. Efe 6:12)—hali hiyo ya ajabu, inayopatikana hata ndani ya moyo wa mwanadamu, ambayo inapinga na kushindana na Mungu. Yesu, na yeye pekee, kupitia kifo chake na Ufufuko wake, ameshinda giza hili na kufungua tena kwa ajili ya wanadamu njia ya kumwendea Mungu, njia ya furaha, haki, na amani. Hivyo, tunaweza kuelewa vipengele vingine vya ujasiri ambavyo Yesu anawaita muwe nao. Ujasiri huu hautokani na azimio lenu wenyewe au nguvu ya tabia yenu. Unatokana na kumwamini Yeye anayewatangulia; unazaliwa kutokana na imani katika Yesu Kristo. Tunapotafakari jinsi Kristo alivyoushinda ulimwengu kwa kuupenda, tunatambua kuwa ujasiri wa Kikristo si ujasiri wa kupinga kitu fulani au mtu fulani, bali ni ujasiri kwa ajili ya kitu fulani: kwa ajili ya uhai, ukweli, uhuru, na haki.
Kwa ujasiri ambao Kristo anatupa, tunaweza kuutazama ulimwengu, ambao Mungu aliupenda sana, kwa mtazamo mpya (taz. Yn 3:16). Sisi pia tuna wajibu wa kutimiza hata kama ni mdogo katika kusaidia kubadilisha “ulimwengu wa giza” kuwa “ulimwengu uliokombolewa.” Kristo hakuiti ili uukimbie ulimwengu huu, bali ili uutazame kwa macho yake na kuugusa kwa upendo wake, ambao huponya kila kitu. Acheni mioyo yenu iguswe na hali halisi inayowazunguka! Yesu hakuupenda ulimwengu akiwa mbali. Aliingia kikamilifu katika hali yetu ya kibinadamu, akajinyenyekeza hata kufikia hatua ya kufa Msalabani (taz. Flp 2:7-8). Alipitia furaha na urafiki, lakini pia magumu, kukataliwa, upweke na mateso, bila hata mara moja kukata tamaa. Wewe pia unaishi katika ulimwengu ulioumbwa ukiwa mwema, lakini uliojeruhiwa—ulimwengu uliojaa fursa, lakini pia wenye dhuluma, mivutano na hofu. Wengi wanatamani amani lakini wanakutana na vurugu; wengi wanatamani ushirika lakini wanapitia upweke. Katikati ya hali hizi zinazokinzana, Wakristo wanaitwa kumfuata Kristo katika ujasiri wake wa upole: ujasiri wa kuonesha upendo wakati ukatili unaonekana kuwa njia rahisi na yenye ufanisi zaidi; ujasiri wa kutafuta amani wakati ugomvi unaonekana kuwa na faida zaidi; na ujasiri wa kushikilia tumaini wakati mtazamo wa kukata tamaa na kutoamini unaonekana kuwa wa kushawishi zaidi.
Ushindi wa upendo wa kujisadaka: Tunaposikia neno “ushindi,” wengine wanaweza kufikiri linamaanisha kuwa na nguvu kuliko wengine, kujitwika mamlaka, au kuhitaji kuthibitisha thamani yetu kila mara. Lakini huo ni aina ya ushindi unaohimizwa na mtazamo wa kawaida wa dunia ushindi wa ulimwengu usio na Mungu. Tunapomwangalia Yesu, tunagundua aina tofauti ya ushindi. Mtakatifu Paulo anatuambia kwamba Kristo, ingawa alikuwa katika umbo la Mungu, alijivua utukufu wake na kuchukua umbo la mtumishi (taz. Flp 2:6-7). Mwana wa Mungu anajinyenyekeza kwa sababu upendo wake unatolewa kwa hiari: hana cha kuthibitisha wala chochote cha kujitafutia ili kujihakikishia usalama. Kwa kujinyenyekeza, hapotezi heshima yake; badala yake, anafunua ukuu na kina cha moyo wake wa kimungu, wenye uwezo wa kutoa uzima kwa wale waliokuwa wamekufa. Ushindi wake ni ushindi wa upendo unaojitoa bila kuhesabu gharama. Vijana wapendwa, ushindi wa kweli haupo katika kutaka kuwashinda wengine, bali katika kujitoa kwa ajili yao. Kwa kufuata njia iliyofunguliwa na Yesu Kristo, nanyi pia hamna haja ya kujilazimisha, kuthibitisha thamani yenu kila mara, kujifanya wakamilifu, au kuficha udhaifu, mashaka, na mapungufu yenu. Kuweni na ujasiri wa kuwa ninyi wenyewe mbele ya Mungu na mbele ya wengine. Heshima yenu haitokani na taswira mnayojijengea. Ninyi ni wa thamani kwa sababu mmeumbwa kwa sura ya Mungu, mnajulikana na Yeye, na mnapendwa na Yeye. Tunagundua sisi ni nani hasa tunapotambua kwamba mioyo yetu iliumbwa kwa ajili ya Mungu: ili kumpenda Yeye, na ndani yake, kuwapenda ndugu zetu. Hakika, ndani kabisa mwetu mna hamu ya kujitoa, ya kuweka maisha yetu kwa ajili ya furaha na ustawi wa wengine. Huu ndio uhuru ambao Kristo anawapa: uhuru wa kutoka katika kujifikiria ninyi wenyewe pekee, na kufungua mioyo yenu kwa ubunifu mkarimu wa upendo.
Ujasiri wa unyenyekevu: Kujitoa kwa Kristo kwa ajili yetu hakukomei Msalabani. Baba anamfufua Mwana kutoka kwa wafu na kumtukuza juu ya viumbe vyote (taz. Flp 2:9-11). Zingatia kwamba Ufufuko si tendo la kujitukuza; bali ni zawadi kutoka kwa Baba na Roho wake Mtakatifu. Hapa tunagundua kipengele kingine cha ujasiri: ujasiri wa kupokea. Tunaweza kukiita ujasiri wa unyenyekevu. Kuwa marafiki wa Yesu kunamaanisha kuzidi kufanana naye zaidi na zaidi katika nyanja hii pia. Kuna mtazamo fulani unaotufanya tuamini kwamba lazima tufanye kila kitu wenyewe, tukijitahidi daima kujiboresha na kujenga utu na tabia imara zaidi. Hata hivyo, mtazamo huu unaweza kutufanya tuamini kwamba sisi ndio waokoaji wetu wenyewe. Injili inatuonyesha njia nyingine ya kukua: si kujiokoa wenyewe, bali kukubali kuokolewa na Yesu Kristo. Hii inahitaji ujasiri wa kukubali msaada kutoka kwa wengine, kutambua mapungufu yetu, kutulia, kusikiliza, na kukabidhi maisha yetu kwa Mungu. Vijana wapendwa, kufungua mioyo yenu kwa Kristo hakutawafanya mpoteze utambulisho wenu. Kinyume chake, mtagundua kwa kina zaidi ninyi ni nani mbele ya Mungu, na mtajijua jinsi Yeye anavyowaona. Hivyo basi, geukieni ndani kabisa ya mioyo yenu. Hamtapotea, kwani huko ndiko Mungu anawangojea. Fungukeni kwa neema yake ya wokovu. Acheni upendo wake yaani Roho Mtakatifu uunde maisha yenu, na mruhusu Yesu akae ndani yenu na kuongoza maamuzi yenu. Hili linapotokea, kila kitu kinakuwa kipya, hata katika mazingira ya kawaida ya maisha ya kila siku: katika uaminifu wenu kwa marafiki, katika heshima kwa wale wenye mitazamo tofauti na yenu, katika kuwajali wale walio wapweke, katika kuwa karibu na wale walio katika mazingira magumu, na hata katika namna mnavyojiendesha katika ulimwengu wa kidijitali. Kila kitu kinabadilishwa na upendo. Wengi huuchukulia upendo kama udhaifu, lakini Kristo anatuonyesha kuwa ni chanzo cha uhuru na nguvu.
Kristo aliyefufuka anakuja kukutana nanyi akiwa na amani yake: Jioni ya Ufufuko, wakati mwanga wa Pasaka ukiwa tayari umeingia ulimwenguni, wanafunzi walikuwa bado wamekusanyika nyuma ya milango iliyofungwa katika Chumba cha Juu, wakiwa wamejaa hofu. Imani haiondoi giza mara moja, lakini pia haituachi peke yetu ndani yake. Yesu, Mshindi, hasubiri wanafunzi washinde hofu yao au wafungue milango. Anakuja katikati yao, na maneno yake ya kwanza ni: “Amani iwe nanyi” (Yn 20:19). Walikuwa wamemwacha. Mmoja alikuwa amemsaliti, na mwingine alikuwa amemkana. Hata hivyo, anawapa amani yake. Labda kuna milango ndani ya mioyo yenu, na katika jamii mnamoishi, ambayo imesalia kufungwa kutokana na kukatishwa tamaa, majeraha, chuki, au hisia za hatia. Kristo anakuja kuwapa amani yake na kuwapatanisha ninyi kwa ninyi. Ujasiri wa Kikristo unatokana na uwepo wa Bwana aliyefufuka, ambaye husamehe na kututuma. Zawadi ya amani yake inatujaza ujasiri ambao ulimwengu hauwezi kuutoa; ujasiri ambao, licha ya majeraha yetu, unafanya hofu isiwe na neno la mwisho tena.
Fungueni mioyo yenu kwa Kristo: Tutakapokusanyika Seoul, mtapata uzoefu wa pekee wa uzuri wa Kanisa la ulimwengu mzima na ukarimu mkuu wa Kanisa nchini Korea. Vijana kutoka mataifa, lugha na tamaduni mbalimbali watakusanyika pamoja, wakiwa wameungana katika Kristo. Kupitia Ekaristi Takatifu, Njia ya Msalaba, Mafundisho ya imani, Maadhimisho ya Liturujia na matukio mengi ya siku hizo, mtatambua upya jinsi Injili inavyovuka mipaka yote na kuzungumza na watu wa kila namna. Acheni siku hizo ziwe tukio la kukutana kweli na Kristo Yesu, fursa ya kukabidhi maisha yenu kwake. Hii ndiyo sababu Siku ya Vijana Duniani ilianzishwa. Hija yetu tayari imeanza. Msizuie maandalizi yenu kwenye mipango ya kiutendaji ya safari yenu kuelekea Seoul pekee: jitayarisheni mioyoni mwenu! Mpelekeeni Kristo maswali yenu na majeraha yenu, lakini pia majeraha yanayovuruga jamii zenu na kusababisha nchi zenu kuwa na uhasama. Mpelekeeni kazi ya uumbaji unaougua na kuteseka, kilio cha Mama Dunia na kilio cha Maskini, ambacho Papa Francisko alitufundisha kukisikiliza. Shirikianeni na Yesu furaha na matumaini yenu. Kwa roho hii, naungana na maneno ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II alitumia kuanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Msiogope! Fungueni milango kwa ajili ya Kristo!” Msingoje hadi muwe wakamilifu ndipo mjifungue kwake. Yeye anakuja kukutana nanyi jinsi mlivyo. Fungueni maisha yenu kwa Kristo. Fungueni jumuiya zenu kwa Kristo. Fungueni njia zinazoelekea kwenye mioyo ya watu mtakaokutana nao. Bwana aliyefufuka, ambaye aliingia kupitia milango iliyofungwa, anaendelea kuja katikati yetu leo. Kwa hiyo, msiridhike na maisha yaliyo chini ya wito ambao Kristo anawaita kuufuata. Acheni muunganishwe na kubadilishwa na upendo wake. Vijana wapendwa, ninatamani sana kukutana nanyi huko Seoul. Lakini kumbukeni: Bwana tutakayekutana naye huko tayari anakuja kukutana nanyi. Pokeeni ahadi yake — “Jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu” (Yn 16:33) na muiruhusu iwe nanyi katika safari yenu yote. Ninawakabidhi kila mmoja wenu kwa maombezi ya kimama ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Na awafundishe, kama yeye mwenyewe alivyofanya, kufungua mioyo yenu kwa Kristo, kutumainia Neno lake na kupokea amani yake kwa furaha, ili mpate kuishiriki na kila mtu. Kutoka Vatican, tarehe 22 Oktoba 2026, Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II.
Friday, November 20, 2026
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments
Post a Comment