Writen by
sadataley
10:27 AM
-
0
Comments
Makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji akoinyesha waraka wa siri wa
CCM unaodaiwa kuandaliwa kwa ajili ya Rasimu ya Katiba inayojadiliwa
Dodoma, alipokuwa akifungua kongamano la wanachama wa chama hicho,
Buguruni jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao
Na Raymond Kaminyoge, MwananchiDar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kitafanya maandamano ya
siku tatu za kazi kupinga kuendelea kufanyika kwa vikao vya Bunge la
Katiba ambayo yatafanyika katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.
Maandamano hayo ni mwendelezo wa hatua ambazo
zimekwishachukuliwa na chama hicho pamoja na vyama vingine vya upinzani
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Aprili 16, mwaka huu, wajumbe kutoka vyama vya
CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi vinavyounda Ukawa walitoka nje ya Bunge
wakidai kuchakachuliwa kwa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko la Katiba.
Jana, uongozi wa CUF uliitisha kongamano la
wanachama wake ili kuwauliza nini kifanyike baada ya wajumbe wa chama
hicho kutoka nje ya Bunge lakini chombo hicho kikapuuza madai yao.
Kongamano hilo lilifunguliwa na makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji
ambaye aliongoza kongamano hilo hadi maazimio hayo yalipotolewa.
Akisoma maazimio ya wanachama baada ya kutoa maoni
yao, ofisa uchaguzi wa CUF, Abdulrahman Lugone alisema wanachama wengi
wameazimia maandamano yafanyike kwa siku tatu katika Mkoa wa Dodoma na
yaishie katika majengo ya Bunge.
“Tunataka maandamano haya yafanyike katika siku za
kazi ili kupeleka ujumbe mzito kwa jamii kwamba maoni yao ndiyo msingi
mkuu wa Katiba,” alisema katika kongamano hilo lililofanyika katika
makao makuu ya chama hicho Buguruni wilayani Ilala.
Alisema pia maandamano hayo yatafanyika siku hiyo
hiyo mkoani Dar es Salaam na kuishia kwenye ofisi ndogo za Bunge ambako
kuna ofisi nyingi za Serikali.
“Tunaomba wafanyakazi na wananchi wanaopinga
kuendelea kufanyika kwa vikao vya Bunge hilo watuunge mkono kwa
kushiriki katika maandamano haya,” alisema.
Lugone alisema vyama vingine vinavyounda Ukawa
vinaombwa siku za maandamano zitakapotangazwa kusitisha shughuli zao ili
wafuasi wake waweze kushiriki kwenye maandamano hayo.
Alisema makao makuu ya chama hicho yanaratibu
maandamano hayo na kwamba wafuasi wa chama hicho watatangaziwa tarehe ya
kufanyika. Wakati kongamano hilo linaendelea makao makuu ya CYF, nje ya
uzio kulikuwa na polisi zaidi ya 25 waliokuwa kwenye magari matatu.
ambao walifika kuanzia saa 5.00 asubuhi na kuondoka saa 7.30 mchana baada ya kumalizika kwa kongamano hilo.
Akifungua kongamano hilo, Duni ambaye pia ni
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, alisema Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameonyesha udhaifu mkubwa katika
kukiongoza chombo hicho.
Alisema udhaifu aliouonyesha katika kusimamia kanuni katika
Bunge hilo ni kielelezo kwamba hana uwezo wa kuwa rais, licha ya
kuonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo.
Sitta amekuwa akitajwa kuwania nafasi ya urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015.
Alisema udhaifu huo ni pamoja na kumpa nafasi
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
kuzungumza kabla ya Rais Jakaya Kikwete katika ufunguzi wa Bunge Maalumu
la Katiba.
“Alitakiwa kuzungumza kwanza Rais Kikwete ndipo
Jaji Warioba angekuwa wa mwisho kutoa hutuba yake lakini Sitta
alichakachua, tunasikitika tulimpa kura nyingi katika uchaguzi wa
kuliongoza Bunge hilo kwa kufuata rekodi za nyuma, lakini ameshindwa
kusimamia kanuni,” alisema Duni.
Akizungumzia mfumo wa serikali tatu, alisema mfumo huo hauwezi kupingwa kwa sababu hayo ni maoni ya wananchi.
“Ikumbukwe kwamba Tume ya Jaji Nyalali
ilipendekeza Serikali tatu, Tume ya Jaji Kisanga pia ilipendekeza
serikali tatu na Tume ya Warioba imetoa maoni ya wananchi waliopendekeza
serikali tatu, hao CCM ni akina nani wanaokataa maoni ya wananchi,”
alihoji Duni.
No comments
Post a Comment