Monday, September 1, 2014

Kocha Phiri apigwa butwaa

Zanzibar. Kocha wa Simba, Patrick Phiri amesema soka la Tanzania limejaa siasa hivyo amewaachia viongozi wa timu hiyo kuamua ni mchezaji gani wa kigeni anafaa kuachwa baada ya kusajiliwa mshambuliaji Emmanuel Okwi.
Juzi jioni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope, alimtangaza rasmi Okwi kuwa mchezaji mpya wa Simba kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Mpaka jana mchana Okwi alikuwa hajajiunga na kambi hiyo iliyopo visiwani hapa huku kukiwapo taarifa kuwa angewasili jana muda wowote.
Simba ilipitisha majina ya wachezaji 28 wakiwamo wachezaji watano wa kigeni ambao ni washambuliaji Amissi Tambwe, Raphael Kiongera, Pierre Kwizera, Joseph Owino na Mosoti.
Usajili wa Okwi katika kikosi hicho unamaanisha kwamba ni lazima mchezaji mmoja wa kigeni akatwe kwani hivi sasa wapo sita na wanatakiwa wachezaji watano tu wa kigeni.
Phiri alisema kuwa mpaka sasa haelewi nini kinaendelea kwani hakushirikishwa katika uamuzi huo hivyo jana Ijumaa alikuwa anasubiri taarifa kutoka kwa viongozi wake juu ya usajili wa Okwi na uamuzi wa mchezaji gani anaondolewa.
“Bado nipo gizani, nimesikia taarifa hizo, lakini nasubiri taarifa ya viongozi, naamini uongozi wa Simba upo vizuri katika kusajili hivyo mchezaji nitakayeletewa atakuwa mzuri maana wao wamemwona na amewahi kuichezea Simba.
“Soka la Tanzania ni kama siasa hivyo tunatakiwa kukubaliana na hali halisi, mimi ni mtaalamu wa benchi la ufundi, lakini viongozi pia wana utaalamu wake, hivyo naamini usajili wao utakuwa mzuri,” alisema Phiri.
Wakati huohuo, Simba leo usiku itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya KMKM kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Hii itakuwa ni mechi yao ya tatu ya kirafiki tangu waingie kambini visiwani hapa ambapo mechi mbili zote walishinda. Mechi ya kwanza walicheza na Kilimani City na kushinda mabao 2-1 wakati mechi ya pili waliifunga Mafunzo bao 2-0.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment