Tuesday, September 9, 2014

TMA imeonyesha njia, wengine waige


Taarifa hizi kuhusu mwelekeo wa mvua kwa miezi ya Oktoba- Desemba zitatufaa sote na hivyo tuzitumie mijini na vijijini kwa ajili ya kupanga na kuandaa mipango yetu ikiwamo safari za nchi kavu, angani au baharini ambazo hakika zitatuepusha na majanga.PICHA|MAKTABA 
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni mojawapo ya wakala za Serikali iliyoko chini ya Wizara ya Uchukuzi ambayo kwa siku za karibuni imejiainisha kwa utendaji mzuri ambao hakuna siri kwamba unafaa kuigwa.
Tuna kila sababu ya kuelezea kuridhishwa na utendaji wa mamlaka hiyo wa kutimiza wajibu wake bila kulazimishwa.
Tunasema mfano huu wa kutoa habari zinazohusu mvua, majanga bila ubabaishaji unaonyesha nia thabiti ya uongozi wake kufanya kazi kwa weledi. Kwa maana hiyo, tunasema hawa wamekuwa mfano wa kuigwa na wengine katika kutimiza wajibu waliokabidhiwa.
Kwa maana hiyo, ni jambo jema kuona mamlaka hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kutoa habari, maelezo na maelekezo kuhusu mwelekeo wa hali ya hewa nchini kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo, kama ambavyo imefanya mwishoni mwa wiki.
Tofauti na siku za nyuma ambako TMA haikuaminika na wakati mwingine kudharauliwa kutokana na taarifa zake nyingi kuwa za kibabaishaji na zisizokuwa sahihi, siku hizi utabiri wake umekuwa wenye uhakika. Sote ni mashuhuda wa jinsi ambavyo mamlaka hii imetabiri kwa usahihi kuhusu majanga, yakiwamo yatokanayo na mvua, vimbunga, upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu na matukio hayo yakawa ya kweli.
Kwa hiyo, hakuna shaka kwamba taarifa hizi kuhusu mwelekeo wa mvua kwa miezi ya Oktoba- Desemba zitatufaa sote na hivyo tuzitumie mijini na vijijini kwa ajili ya kupanga na kuandaa mipango yetu ikiwamo safari za nchi kavu, angani au baharini ambazo hakika zitatuepusha na majanga.
Kikubwa zaidi, taarifa hizi zinahusu sekta mtambuka, hivyo lazima ziheshimiwe, zitumiwe vizuri na kila mmoja wetu katika kupanga shughuli zetu zikiwamo kilimo, ufugaji, matumizi ya maji na nyinginezo.
Tunashauri pia kwamba taarifa hizi zitumiwe kwa manufaa badala ya kupuuzwa kama ambavyo imekuwa ikifanyika. Tunafahamu, kwa mfano kilimo chetu ni chenye kutegemea mvua katika maeneo mengi nchini , hivyo wakulima wanazitegemea taarifa kama hizi kwa maisha yao ya kila siku ili kuchagua aina ya mazao wanayopaswa kulima.
Kwa maana hiyo, yatakuwa makosa makubwa kupuuza utabiri kama huu na matokeo yake nchi yetu kujikuta katika majanga kama ya ukame, upungufu wa chakula na mafuriko.
Tunasema ushauri wa TMA hauna budi uzingatiwe na kila mmoja wetu, ikiwa ni pamoja na wakulima, wataalamu katika sekta mbalimbali na watunga sera, hasa ikizingatiwa kuwa ushauri unatolewa bure, tena kwa lugha nyepesi.
Kama tulivyosema hapo juu, utabiri huo una lengo la kutupatia taarifa muhimu ambazo hatimaye zitatuepusha na maafa. Hivyo, taarifa hizo zikifanyiwa kazi, zitatuondoa katika majuto, hasara na mateso mengi ambayo yamekuwa yakitupata au mtu mmoja mmoja.
Kwa mfano, wakazi wa mabondeni kila mwaka hutaabika wakati wa masika, huishi kwa hofu kutokana na kutopata taarifa hizo na wakati mwingine kutoheshimu utabiri kama huo.
Tunazishauri idara nyingine za Serikali, hasa zenye wasemaji walioajiriwa kwa kazi hiyo, lakini wameshindwa kutoa taarifa muhimu kwa umma, waige mfano wa wenzao katika TMA.
Tunazishauri idara hizo za Serikali ambazo badala ya kuwa sehemu ya vyanzo vya habari, zimekuwa zikificha habari, zitambue kuwa jambo hilo kamwe halikubaliki.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment