Writen by
sadataley
3:36 PM
-
0
Comments
Papa Francisko: Miaka 4 ya Kumbu kumbu ya kuchaguliwa kwake!
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anampongeza Baba
Mtakatifu Francisko kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 4 tangu
alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na tangu mwanzo amejipambanua
kuwa ni mtu wa watu mintarafu hotuba yake ya mwanzo kabisa, aliyoonesha
na kushuhudia: amani na utulivu wa ndani; upole na unyenyekevu kiasi cha
kuomba sala kutoka kwa watu wa Mungu ili waweze kumsindikiza katika
maisha na utume wake. Tangu wakati huo, Baba Mtakatifu aliwataka waamini
kutembea kwa pamoja kwa kujiaminisha katika sala na huruma ya Mungu.
Ikumbukwe kwamba, Papa Francisko hakuwa kati ya Makardinali waliokuwa
wanatajwa sana na vyombo vya habari kuwa wangeweza kuchaguliwa
kuliongoza Kanisa Katoliki baada ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuamua
kung’atuka kutoka madarakani! Katika mahojiano maalum na Radio Vatican,
Kardinali Parolin anakaza kusema, Baba Mtakatifu anapenda kuendeleza
safari ya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo,
iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kweli
zile cheche za mageuzi zilizoletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa
Vatican ndani ya Kanisa ziweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya
watu! Kanisa halina budi kufanya hija ya kumwelekea Kristo Yesu, huku
likiwasaidia watu kukutana na watu, ili kwa pamoja waweze kusonga mbele!
Hii ndiyo dhana ya Sinodi inayopewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu
Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa halina budi
kuwaambata wote kwa kujiaminisha chini ya ulinzi, tunza, uongozi na
karama za Roho Mtakatifu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya
huruma umelisaidia Kanisa kurejea tena katika mhimili wa maisha na utume
wake yaani huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika historia nzima
ya ukombozi wa mwanadamu! Kumbe, Kanisa linapaswa kuwa ni chombo na
shuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi. Malango ya huruma
ya Mungu yamefungwa kwenye Majimbo mbali mbali, lakini Mlango wa huruma
ya Mungu ambaye ni Kristo Yesu, bado uko wazi kwa wale wanaotaka kutubu
na kumwongokea Mungu ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na
kifani!
Kardinali Parolin anasema, Maadhimisho ya Mwaka Huruma ya Mungu imekuwa
ni fursa kwa waamini kutambua umuhimu wa Sakramenti za huruma ya Mungu
yaani: Ekaristi Takatifu na Kitubio. Kumekuwepo na mwamko mkubwa kwa
waamini kukimbilia huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho
sehemu mbali mbali za dunia, jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na
utume wake umuhimu wa upendo na mshikamano wa huduma makini kwa maskini
na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kipindi hiki cha
Kwaresima mwaliko ni kutubu na kumwongokea Mungu; kusali, kutafakari,
kufunga na kujinyima; yote haya yanamwilishwa katika matendo ya huruma:
kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa kweli ni
mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma ya upendo wa kidugu kwa
maskini ni utambulisho makini wa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia.
Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, Wosia wa Kitume wa Baba
Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya
familia” ni zawadi kubwa kwa waamini katika mchakato mzima wa kutangaza
na kushuhudia Injili ya familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha
ya mwanadamu. Familia inakabiliana na changamoto nyingi ambazo ni
matokeo pia ya dhambi ya asili ambayo imemwachia mwanadamu majeraha
makubwa katika maisha yake. Wosia huu ni chachu ya mageuzi katika maisha
na utume wa familia. Shutuma na hali ya kutoelewana ni sehemu ya safari
ya maisha ya Kanisa hapa duniani! Baba Mtakatifu Francisko anasema,
anakubali kukosolewa, lakini ukosoaji huu uzingatie ukweli, hali na
huruma ya Mungu kwa binadamu, ili hatimaye, kuweza kusoma alama za
nyakati na utashi wa Mungu, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha
ya binadamu.
Kardinali Parolin anasema, moyo wa binadamu ni kiini cha mageuzi
yanayotekelezwa na Mama Kanisa na kwamba, Kanisa daima liko katika
mchakato wa mageuzi yanayojikita katika toba na wongofu wa ndani, ili
kuliweza Kanisa kujizatiti zaidi katika maisha na utume wake. Katika
kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko,
kumekuwepo na maamuzi makubwa yaliyofanyika na kutekelezwa, lakini haya
ni mageuzi ambayo yanapaswa kupata chimbuko kutoka katika undani wa
maisha ya familia ya Mungu. Lengo ni kuwawezesha waamini kurejea katika
mambo msingi ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kumwongokea Mwenyezi
Mungu, ili kutangaza na kushuhudia asili na kiini cha Kanisa.
Kardinali Parolin anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kuwa karibu
zaidi na Papa Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro anayeendelea kushuhudia kwa walimwengu utajiri mkubwa wa
amani, utulivu wa ndani, furaha na ucheshi hata pale anapokabiliwa na
matatizo na changamoto katika maisha na utume wake kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro. Kuna changamoto nyingine ni kubwa kiasi hata cha
kutishia maisha, lakini bado Papa Francisko anayaangalia matukio yote
haya kwa amani na utulivu wa ndani sanjari na kuendelea kujiaminisha
katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo
kwa wale wanaomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Yote haya
anasema Kardinali Pietro Parolin katika mahojiano maalum na Radio
Vatican, Papa Francisko anapoadhimishwa kumbu kumbu ya miaka 4 tangu
achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki yanampatia faraja, imani na
matumaini ya kuendelea kusonga mbele katika maisha na utume wake, kama
Katibu mkuu wa Vatican.
Chanzo:tec1956.blogspot.com

No comments
Post a Comment